September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi hakikisheni mnapata hati

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

WANANCHI wa Kata ya Nyasaka na Jimbo zima la Ilemela wametakiwa kuhakikisha wanapata hati miliki za viwanja vyao ili kuwa salama na kuweza kufanyia shughuli za kiuchumi na maendeleo kwakuwa ardhi ni muhimu na msingi wa uchumi.

Wito huo umetolewa na Mgombea Ubunge Jimbo la Ilemela kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Angeline Mabula katika mkutano wake wa 31 wa muendelezo wa kampeni za kumnadi mgombea Ubunge huyo na wengine wa CCM uliofanyika Nyasaka Centre Kata ya Nyasaka.

Amesema, Serikali ya Awamu ya Tano kwa vile inawajali wanyonge, iliamua kurasimisha makazi na kupimia wananchi maeneo yao hata wale waliokuwa wamefanya ujenzi holela.

Dkt. Angeline amesema, wale wote ambao wamepimiwa ardhi zao waende kuchukua hati zao kwani ndio salama ya miliki yao na kuweza kufanyia shughuli za kimaendeleo kwani huwezi kuwa na migogoro na jirani yako sababu kila mtu anajua mipaka yake na ramani inakua inaonyesha, kuwekewa vigingi tu haitoshi kwani kuna watu ambao siyo waaminifu wanaving’oa hivyo kufanya mhusika kutokuwa na uhakika wa kiwanja chake kuwa kimeishia wapi.

Amesema, sekta ya ardhi katika suala la urasimishaji makazi na umilikishaji wa ardhi kwa miaka mitatu mfululizo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imeongoza ambapo kwa asilimia 90 kazi imefanyika na imebaki asilimia 10 tu ili upimaji ukamilike.

Meneja Kampeni wa CCM Jimbo la Ilemela Kazungu Idebe (katikati) akimnadi kwa wananchi wa Kata ya Nyasaka mgombea Ubunge Jimbo la Ilemela kupitia CCM Dkt. Angeline Mabula(kushoto) na Diwani wa Kata ya Nyasaka, Abdulhahman Simba (kulia) kwenye mkutano wa kampeni wa kuomba kura kwa wananchi uliofanyika Kata ya Nyasaka. (Picha na Judith Ferdinand).

“Leo ninapoongea maeneo ya Nyasaka yamepimwa kwa kiasi kikubwa sana,viwanja 8069 vimepimwa kati ya hivyo 6003 wamechukua hati, niwaombe ambao mmeisha kamilisha upimaji chukueni hati kwani ukipimiwa na usichukue hati yako,sawa sawa kuwa na ardhi isiyokuwa na faida,ongezeko la thamani la ardhi yako ni pale unapo kamilisha kupimiwa na kupewa hati yako,ukipewa hati yako umeisha wezeshwa kiuchumi kwani unaweza kuitumia kukopa benki kwa kuweka dhamana na uhakika na salama ya miliki yako,” amesema Dkt. Angeline.

Amesema, migogoro mingi ya ardhi iliyokuwa ikikabili jimbo la Ilemela na kupelekea kukwama kwa baadhi ya shughuli za maendeleo ikiwemo kuendeleza ardhi za wananchi kwa asilimia 90 imeweza kutatuliwa kupitia Serikali ya CCM chini ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt.John Magufuli.

Katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake amefanikiwa kusaidia utatuzi wa migogoro mikubwa ya ardhi iliyokuwa ikisumbua wananchi wa jimbo hilo ikiwemo ule wa wananchi na Jeshi la Polisi katika eneo la Kigoto Kata ya Kirumba, mgogoro wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ) na wananchi wa Lukobe, Buduku Kata ya Kahama, mgogoro ardhi kati ya wananchi wa Nyagunguru na Jeshi la Wananchi Kata ya Ilemela, huku mgogoro wa wananchi na Mamlaka ya Uwanja wa ndege wa Mwanza ukisubiria maamuzi ya Rais kwa utatuzi wa mwisho.

“Suala la ardhi linachangamoto namshukuru Mungu wakati naingia madarakani alipenda nipewe eneo hili lakini ni eneo lenye changamoto kwa sababu sikua pekee Mungu alikua pamoja na mimi lakini na watanzania walionipa dhamana na kunifanya niwe Mbunge wao na Rais akanipa dhamana ya kumsaidia katika sekta ya ardhi ambao ni mfupa wa fisi wengi uliwashinda kutatua namshukuru Mungu mpaka leo Ilemela ni vinara na migogoro ya ardhi tumelishughulikia kwa zaidi ya asilimia 90 na mingi tumeimaliza,haiwezekani niwe Naibu waziri wa ardhi alafu kwangu kuongoze kwa migogoro,” amesema Dkt Angeline.

Meneja Kampeni wa CCM Jimbo la Ilemela Kazungu Idebe amesema, wagombea wanaotokana na CCM wametokana na chama chenye misingi,ilani na historia na maono ambapo kimejipanga katika kuwaletea maendeleo wananchi hivyo wawapigie kura wagombea wanaotokana na chama hicho waweze kusukuma maendeleo kwa kasi zaidi.

“Dkt. Magufuli mwaka 2015 wakati anaingia madarakani walimfunga injini ya scania katika uchaguzi huu
kwa marefu na mapana anaenda kutekeleza ilani yenye ukurasa zaidi ya 300 hivyo tumeamua kumfungua injini ya scania na kumfungia ya trekta na anavinasaba vya kufanana na watanzania ambaye anaweza kutetea wananchi kwa kushirikiana na Mbunge na Diwani wanaofanana yani wa CCM ambapo kwa kipindi cha miaka mitano amefanya makubwa ikiwemo sekta ya elimu, afya, ardhi, maji na umeme,” amesema Idebe.