November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

KMC: Tutarudi kwenye makali yetu

Na Angela Mazula, TimesMajira Online

BAADA ya kupoteza michezo miwili mfululizo ya Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), benchi la ufundi la timu ya KMC limeweka wazi kuwa wanakwenda kujipanga ili kurudi katika makali waliyoanza nayo mwanzo mwa msimu.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Habari wa klabu hiyo, Christina Mwagala mara baada ya mchezo wao wa juzi uliochezwa kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam dhidi ya Maafande wa Polisi Tanzania ambao walikubali kichapo cha goli 1-0 lililofungwa dakika ya 87 na Pius Buswita.

Kabla ya mchezo huo, KMC pia walipoteza mbele ya wenyeji wao Kagera Sugar katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Kaitaba, Septemba 25.

Baada ya matokeo hayo mikakati ya benchi la ufundi la timu hiyo ni kutumia muda huu wa mapumziko mafupi ya kupisha maandalizi ya timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ambayo itakutana na Burundi katika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki utakaochezwa Oktoba 11.

Amesema, kama waliweza kuanza Ligi vizuri kwa kushinda mechi tatu mfululizo na kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi, wana uhakika wataweza kurudi kwenye makali baada ya mapumziko kumalizika.

“Baada ya kupoteza mechi zetu mbili, sasa tunakwenda kufanya marekebisho katika kipindi hiki cha mapumziko hivyo tunauhakika Ligi itakaporejea tutakuwa tumesharudi kwenye ubora wetu kwani benchi la ufundi pamoja na wachezaji wote wapo vizuri hivyo mashabiki wetu wasikate tamaa kwani bado tuna mechi nyingi mbele yetu, ” amesema Mwagala.

Katika maandalizi watakayoendelea nayo baada ya mapumziko ya siku chache ya wachezaji, yatajikita zaidi katika mbinu ambazo zitawapa ushindi dhidi ya Coastal Union ambao watakutana nao Oktoba 14.