May 30, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC akemea uvuvi haramu

Na Fresha Kinasa ,Times Majira Online,Mara.

MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amewaonya wanaojihusisha na uvuvi haramu kuacha mara moja vitendo hivyo, akisema serikali ya mkoa huo imeimarisha ulinzi kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria.

Kanali Mtambi ametoa kauli hiyo Mei 30, 2026, alipokuwa akizungumza katika bonanza la michezo la watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS) kwa mikoa saba ya Kanda ya Ziwa, lililofanyika katika Uwanja wa Karume uliopo Maniapaa ya Musoma.

Amesema kuwa, uvuvi haramu haukubaliki kwa namna yoyote ile na kuwatahadharisha wanaojihusisha na shughuli hizo kuziacha mara moja, kwani serikali itachukua hatua kali za kisheria dhidi yao.

Aidha, Kanali Mtambi amevipongeza vyombo vya usalama, wananchi wa Mkoa wa Mara na wadau mbalimbali kwa mchango wao uliosaidia kupungua kwa makosa ya jinai mkoani humo.

Ameeleza kuwa, mafanikio hayo yametokana na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi pamoja na uimara wa vyombo vya usalama katika kuimarisha ulinzi na usalama kwa ajili ya maendeleo ya mkoa.

Amewataka wananchi wa Mkoa huo, kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano, sambamba na kufanya kazi halali kwa bidii ili kujiletea maendeleo.

Juma Shadrack, ni Mkazi wa Kata ya Bweri, amewahimiza Wananchi wanaojishughulisha na uvuvi kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Mkuu huyo wa Mkoa. sambamba na Kuunga mkono juhudi za serikali katika kutokomeza vitendo vya uvuvi haramu, kwa manufaa endelevu.