Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
UMOJA wa wanawake kutoka vyama 12 vya siasa nchini umelaani matukio ya utekaji yanayoendelea nchini na kuiomba Serikali kuunda Tume maalum ya uchunguzi ili kubaini chanzo cha matukio hayo ambayo yamekuwa yakisababisha hofu katika jamii.
Vyama vilivyoshiriki katika umoja huo ni Tanzania Labour Party (TLP), Chama cha Kijamii (CCK), Chama cha Demokrasia (DP), National Reconstruction Alliance (NRA), Sauti ya Umma (SAU), UMD, United Democratic Party (UDP), NCCR-Mageuzi, AAFP, ADA-TADEA, Chama cha Demokrasia Makini pamoja na UPDP.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mei 26, 2026, viongozi hao wa wanawake wamesema kuna umuhimu wa Serikali kuongeza juhudi za kuimarisha usalama wa wananchi na kuhakikisha wahusika wa vitendo vya utekaji wanabainishwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Mwenyekiti wa Wanawake Taifa wa Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Rachel Balama, amesema matukio hayo yameendelea kuzua hofu kwa wananchi hivyo hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa kudhibiti hali hiyo.
Amesema miongoni mwa hatua zinazopaswa kupewa kipaumbele ni kufungwa kwa kamera za CCTV katika maeneo muhimu ya mijini pamoja na kuongeza matumizi ya teknolojia za kiusalama ili kusaidia kuwabaini wahalifu kwa haraka kabla na baada ya matukio ya uhalifu kutokea.
“Tunaiomba Serikali kuunda Tume maalum ya uchunguzi ili kubaini chanzo cha matukio haya ya utekaji na mauaji na kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria,” amesema Balama.

Kwa upande wake, Mratibu wa Chama cha NLD Taifa, Mwajuma Mirambo, amesema Serikali inapaswa kuongeza jitihada za makusudi katika kuboresha afya ya mama na mtoto kutokana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika sekta hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Wanawake wa Chama cha DP, Rehema Shauri, amesema wanawake wana wajibu mkubwa wa kulinda amani ya nchi kwa kuwa ndio walezi wakuu wa familia na msingi wa malezi katika jamii.
Amesema ushiriki wa wanawake katika masuala ya amani na maendeleo ni muhimu katika kujenga taifa lenye mshikamano, utulivu na usalama.

More Stories
Taasisi ya OSHA yapata Bodi mpya
Rafiki wa Binti wafanya kweli Afya ya Hedhi
Mke adaiwa kumuua Mumewe kwa sindano yenye sumu