May 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi ya OSHA yapata Bodi mpya

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu ameitaka Bodi Mpya ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa na Taasisi hiyo katika kutekeleza jukumu lake la msingi la kulinda nguvukazi ya Taifa kupitia usimamizi wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Sura Na. 297, Toleo la 2023.

Waziri Sangu ametoa wito huo katika hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Saba ya OSHA iliyofanyiaka katika Ofisi za OSHA Jijini Dar es Salaam Mei 25, 2026 Jioni.

“OSHA ni miongoni mwa Taasisi zinazofanya vizuri kwasasa hususan katika kutoa miongozo na ushauri kwa wamiliki wa sehemu za kazi juu ya uboreshaji mazingira yao na kuimarisha afya za wafanyakazi,” ameeleza Waziri Sangu na kuongeza:

“Wengi wetu tumeshuhudia siku za hivi karibuni mabenki na Taasisi nyingine wamekuwa na programu nyingi za mazoezi zinazolenga kuimarisha afya za wafanyakazi pamoja na kuchochea ari ya kufanya kazi. Kimsingi programu hizi ni matokeo ya ushauri wa wataalam wa OSHA baada ya takwimu zao za uchunguzi wa afya za wafanyakazi kuonesha wafanyakazi wengi wanakabiliwa na changamoto za magonjwa yasiyoambukiza.”

Amebainisha kwamba Bodi hiyo imekuja wakati muafaka kutokana na kuanza majukumu yake ikiwa miongozo yote muhimu ikiwemo; Dira ya Taifa ya mwaka 2050, Mpango wa Maendeleo wa Taifa, Ilani ya Chama Tawala pamoja na Mpango Mkakati mpya wa Taasisi ya OSHA ambao utaanza kutumika Julai mwaka huu.

Aidha, ameitaka Bodi kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya weledi ikiwa ni pamoja na kujikita katika majukumu yao ya msingi ambayo ni kusimamia sera na maono ya Taasisi katika mawanda mapana badala ya kujikita katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Taasisi ambayo ni kazi ya Menejimenti.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Bodi, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Makwaia Makani, amesema Bodi yake imepokea jukumu walilopewa kwa mikono miwili na imejipanga kutoa ushauri wa kitaalam na kimkakati ili kuiwezesha Taasisi ya OSHA kupata mafanikio zaidi.

“Mheshimiwa Waziri, naomba nikuhakikishie kwamba tutafanya kazi kwa mshikamano, uwazi na uwajibikaji mkubwa na tutaisadia menejimenti ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo,” ameeleza Makani.

Awali, akitoa maelezo kuhusu Taasisi ya OSHA katika hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema menejimenti ya OSHA imefarijika kupata Bodi Mpya baada ya Bodi iliyokuwepo kumaliza muda wake.

“OSHA ina menejimenti nzuri sana inayofanya kazi kwa kuzingatia misingi ya weledi na kujituma hivyo tupo tayari kupokea ushauri na maelekezo ya Bodi na kuyatekeleza ipasavyo ili Taasisi yetu iweze kusonga mbele,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa OSHA.

Wajumbe wa Bodi ya Saba ya Ushauri ya OSHA ni pamoja na; Makwaia Makani (Mwenyekiti),Rehema Ludanga (Mjumbe), Renatus Mbamilo (Mjumbe),Mercy Sila na Lilian Francis (Mjumbe).