May 25, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watuhumiwa kulima bangi zaidi ya ekari 10

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Sengerema

WATU wawili wilayani Sengerema mkoani Mwanza, wanashikiliwa kwa tuhuma za kujihusisha na kilimo cha bangi kwenye shamba lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 10, pamoja na kukutwa na shehena za zao hilo haramu ikiwa imeshafungashwa kwa ajili ya kusafirishwa kwenda maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza jijini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa,amesema Mei 23, 2026, majira ya mchana,jeshi hilo lilipokea taarifa kutoka kwa wananchi wema zikieleza uwepo wa shamba hilo kubwa la bangi katika Kitongoji cha Nyerere, Kijiji cha Busekeseke kilichopo Tarafa ya Buchosa, wilayani Sengerema.

DCP.Mutafungwa amesema baada ya kupokea taarifa hizo, askari polisi walifika eneo la tukio mara moja na kufanikiwa kumkamata mmiliki wa shamba hilo, aliyefahamika kwa jina la Mudumuka Kabika (60) maarufu Ziliona Tibakula, ambaye ni mkazi wa eneo hilo.

Amesema,katika misako huo walifanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa wa pili aliyefahamika kwa jina la Mawazo Manisha(50) mkulima na mkazi wa Kijiji cha Busekeseke, akiwa eneo la tukio ambapo alikutwa na mafurushi ya bangi yaliyokuwa tayari kwa ajili ya kusafirishwa.

Pia amesema wakati wa operesheni hiyo, askari walibaini uwepo wa magunia na vifurushi vingine vilivyokuwa vimeandaliwa kwa ajili ya kufungasha zao hilo haramu, huku sehemu kubwa ya shamba hilo ikiwa bado imesheeni mmea huo uliopigwa marufuku kisheria.

“Hivi sasa watuhumiwa wote wawili wanashikiliwa na jeshi la polisi, wanaendelea kuhojiwa kwa kina, na taratibu zote za kisheria zikikamilika watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo ili kujibu tuhuma zinazowakabili,”amesema DCP.Mutafungwa.

Haya hivyo DCP.Mutafungwa,amesema oparesheni hiyo ni muendelezo wa mikakati thabiti na endelevu ya jeshi hilo katika kudhibiti na kutokomeza kilimo, mtandao wa usafirishaji, pamoja na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Hata hivyo ametoa onyo kwa jamii kuacha mara moja kujihusisha na kilimo cha bangi na badala yake wajikite kwenye kilimo cha mazao halali ya chakula na biashara yatakayowaletea maendeleo.

Sanjari na hayo amewataka viongozi wa Serikali za Mitaa na wananchi kwa ujumla kuacha kufanya siri na badala yake waendelee kutoa ushirikiano wa karibu kwa kufichua vitendo vya uhalifu katika maeneo yao.