May 25, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MNEC Mwaselela: Samia ana dhamira kwa vijana

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

VIJANA wametakiwa kutumia fursa zinazotolewa na serikali kwa maendeleo yao na taifa, huku wakihimizwa kudumisha amani, uzalendo na mshikamano wa kitaifa.

Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM taifa (MNEC), Ndele Mwaselela, amesema hayo wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la Jumuiya ya wanafunzi wa kiislamu wa vyuo vikuu na vyuo vya kati (TAMSYA) lililofanyika Jijini Mbeya, Mwaselela amesema Rais Samia ameendelea kuweka mazingira rafiki na kuandaa fursa mbalimbali kwa vijana ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.

Amesema viongozi wameelekezwa kuwa karibu na vijana ili kusikiliza changamoto zao na kuwapa moyo wa kutumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo. Aidha, amesema Rais Samia anaendelea kuijenga Tanzania yenye matumaini kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

“Rais Samia ana dhamira ya kweli, maono, ndoto na upendo mkubwa kwa vijana wa nchi hii…..hivyo vijana hatuna budi kumuunga mkono katika juhudi za kuleta maendeleo katika taifa hili”amesema Mwaselela

Mwaselela amesema vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda amani, umoja na utulivu wa nchi kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa. Amesema bila amani na mshikamano, maendeleo hayawezi kupatikana kwa urahisi.

Akitoa ushuhuda wa maisha yake, Mwaselela amesema ametoka katika mazingira ya kawaida lakini mafanikio yake yametokana na juhudi, uthubutu na kutokata tamaa na kuwa wazazi wake walifanya kazi za kawaida huku yeye akisoma katika mazingira yenye changamoto kama vijana wengi wa sasa.

Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Msafiri Njalabaha amesema kongamano hilo limekuwa chachu ya kuwajenga vijana katika maadili, elimu na imani, huku akiwataka kutumia vizuri mitandao ya kijamii kwa maendeleo yao.

Naye katibu mkuu wa TAMSYA mkoa wa Mbeya, Abdalahaman Abdalah amesema kongamano hilo limewakutanisha wanafunzi 150 kutoka vyuo mbalimbali kujadili elimu, maadili na maendeleo ya vijana.

Amesema serikali imeongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu hadi Sh Bil. 700 katika mwaka wa fedha 2024/2025, hatua iliyoongeza wanufaika hadi wanafunzi 220,000 na kuwapa matumaini vijana wengi kuendelea na masomo yao.