September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baadhi ya Maafisa kutoka Idara na Taasisi mbalimbali wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt Bilinith Mahenge wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani yaliyofanyika jijini Dodoma.

Siku ya Makazi Duniani itumike kuboresha makazi

Na Munir Shemweta

DESEMBA mwaka 1985 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia Azimio Na 40/202 liliazimia kuwa kila Jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba kila mwaka itakuwa ni siku maalum ya kuadhimisha masuala ya makazi duniani. Siku hiyo hujulikana kote duniani kama siku ya makazi Duniani.

Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Willium Lukuvi

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa chini ya utaratibu wa Shirika la Makazi Duniani (UN-HABITAT) kuadhimisha siku hii kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutafakatri hali ya makazi katika nchi na changamoto zake husika na kupanga mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo. Kila tarehe 5 ya kwanza ya mwezi Oktoba Tanzania inajumuika na jumuiya ya kimataifa kuadhimisha siku ya Makazi Duniani.

Maadhimisho ya Siku ya Makazi duniani yanatoa fursa kwa kila taifa wananchi na wadau wengine wa makazi kutafakari kila mmoja kwa nafasi yake namna atakavyoshiriki kuboresha hali ya makazi katika miji yetu.

Tanzania kama nchi na jamii inapaswa na ina wajibu wa kujiandaa kwa maisha ya kijamii zaidi. Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa maeneo mengi ya miji yanazidi kuongezeka kwa ukubwa na idadi ya wakazi na vijiji vinakua na kugeuka kuwa miji.

Baadhi ya Maafisa kutoka Idara na Taasisi mbalimbali wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Bilinith Mahenge wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani yaliyofanyika jijini Dodoma.

Siku ya Makazi Duniani inaongozwa na Kauli mbiu ya mwaka husika. Kauli mbiu huwezesha kutafakari suala husika kwa kina. Hutoa fursa ya kujiwekea nafasi na mazingira wezeshi ya kutafuta ufumbuzi wa muda mfupi, wa kati na muda mrefu wa suala husika kwa mwaka huo. Kauli mbiu ya mwaka huu ni Nyumba kwa wote Miji bora ya Baadaye.

Nyumba ni mojawapo ya mahitaji ya msingi ya binadamu. Haki ya kila mtu kuwa na nyumba bora inatambuliwa kitaifa na kimataifa. Yapo matamko na mikataba inayotambua haki hii ya msingi kama vile Universal Declaration of Human Rights ya mwaka 1948 na ya mwaka 1966.

Kwa kutambua haki hiyo Tanzania imeridhia mkataba na tamko hilo. Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000 pia inatoa mwongozo kuipa kipaumbele sekta ya nyumba katika kuwezesha upatikanaji wa nyumba bora na za gharama nafuu kwa wananchi wa vipato mbalimbali.

Nyumba pia ni kigezo kikuu cha kukuza uchumi na kudumisha amani katika nchi yoyote duniani. Uwekezaji katika sekta ya nyumba unachangia moja kwa moja kwenye ukuaji mitaji, ajira, kipato, akiba na kuimarisha afya na elimu.

Serikali zote duniani zinathamini mchango wa sekta ya nyumba katika kukuza uchumi na kichocheo katikam kudumisha amani. Hivyo ni dhahiri kwamba hakuna nchi inayoendelea bila kutoa kipaumbele katika sekta ya nyumba.

Ukuaji wa sekta ya nyumba nchini unachangiwa na uwekezaji unaofanywa na serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi. Pamaoja na sekta hii kukua taratibu zipo jitihada kadhaa ambazo serikali imezifanya katika kuhakikisha kuwa sekta hii inakuwa hapa nchini na jitihada hizo ni pamoja na kuanzishwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Benki ya Nyumba Mfuko wa mikopo ya Nyumba kwa watumishi wa Serikali na kuanzishwa Kampuni ya Watumishi Housing (WHC).

Aidha,juhudi nyingine ni kutungwa kwa sheria kadhaa kama vile sheria ya mikopo ya nyumba (Mortage Financing Special Provision Act, 2008,Sheria ya Miliki ya sehemu ya Jengo (The Unit Titles Act, 2008) sambamba na uanzishwaji miradi na mifuko mbalimbali katika kusaidia kuwezesha maendeleo ya sekta ya nyumba kama vile mradi wa mikopo ya nyumba (Housing Finance Project), Mfuko wa mikopo midogomidogo ya nyumba (Housing Micrifinance Fund-HMFF).

Kupitia mradi ya mikopo ya nyumba (Housing Financing Project) ambapo chini ya mradi huo mabenki na taasisi za fedha zimekuwa zikipatiwa mitaji kwa ajili ya kutoa mikopo ya nyumba kupitia Tanzania Mortagage Refinance Company (TMRC) na hivyo kuimarisha upatikanaji mikopo ya ujenzi au ununuzi wa nyumba na hadi sasa Serikali ya awamu ya tano imetoa mikopo isiyopungua bilioni 438.58 na wananchi wapatao 5,460 wamenufaika na mikopo kwa utaratibu huo.

Serikali katika kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye sekta ya nyumba na kuwezesha mazingira ya upatikanaji nyumba za gharama nafuu ipo katika hatua mbalimbali za kuandaa Sera Mpya ya Nyumba. Sera hii itatoa dira ya uendelezaji wa sekta ya nyumba nchini. Juhudi zitaelekezwa katika kubuni mbinu mbalimbali za kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kupata nyumba zilizo bora.

Aidha,Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI itaendelea kutekeleza miradi ya urasimishaji nchini kwa kutambua miliki hatua kwa hatua ili kuyaweka maeneo yenye makazi holela huduma za kiuchumi na kijamii kupitia mpango shirikishi.

“Miradi hii itaendelea katika miji mbalimbali nchini kwa lengo la kuboresha hali ya maisha ya makazi husika na kupunguza umasikini, faida nyingine ni pamoja na kuongeza usalama wa miliki kwa kutoa hati miliki za ardhi” anasema Waziri wa Ardhi William Lukuvi.

Katika salamu zake za siku ya Makazi Duniani, Lukuvi anasema, Wizara ya Ardhi iko katika maandalizi ya kufanya sensa ya nyumba ili kutambua idadi kamili ya nyumba na kusaidia kubaini uhaba na hali ya nyumba na kusisitiza kuwa matokeo ya sensa hiyo yatasaidia kuandaa mipango mikakati ya maendeleo ya nyumba.

Katika kinachooneka kuzingatia umuhimu wa nyumba kwa kila mwananchi, Lukuvi aliziagiza ofisi za ardhi katika mikoa yote pamoja na mamlaka za upangaji kusimamia kikamilifu zoezi la utambuzi , upangaji, upimaji na umilikishaji wa makazi kwa kufuata sheria , kanuni, taratibu na miongozo iliyotolewa ili kila mwananchi mwenye kiwanja na nyumba sehemu zinazokubalika kisheria aweze kumilikishwa.

Aidha,alizitaka halmashauri zote kuwapatia waendelezaji miliki huduma watakazohitaji kama vile kuanisha maeneo yaliyoiva kimipango miji, kuandaa miapango ya uendelezaji miji, kupima viwanja na kuweka miundombinu na kuongeza kuwa halmashauri pia zinapaswa kutoa hati miliki za ardhi na vibali vya ujenzi kwa wakati bila kusahau jukumu lao la msingi la kussimamia na kukagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alihitimisha salamu zake za siku ya Makazi Duniani kwa kuwataka wananchi kuitumia siku hiyo kutafakari mada mbalimbali na kuzijadili kwa kina kuona ni jinsi gani zinaweza kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika masuala ya sekta ya maendeleo ya nyumba nchini.