


Na Joyce Kasiki, Dodoma
WADAU wa sekta ya milki nchini wameiomba Serikali kuharakisha maboresho ya sheria za usimamizi wa sekta hiyo ili kudhibiti ongezeko la madalali wa ardhi wasiokuwa na usajili rasmi wanaosababisha wananchi kupata hasara huku Kamishna wa Ardhi, Nathaniel Nonge akisema Serikali ipo tayari kushirikiana na wadau kuhakikisha sekta ya milki inakuwa salama, yenye tija na inayolinda maslahi ya wananchi pamoja na wawekezaji.
Akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka na Kongamano la Chama cha Wataalamu wa Sekta ya Milki Tanzania (AREPTA) unaoendelea jijini Dodoma mwaka 2026 amesema una lengo la kujadili maendeleo na changamoto zinazoikabili sekta ya milki nchini.
Rais wa AREPTA, Boniphace Yumba, amesema bado kuna changamoto kubwa ya baadhi ya madalali kufanya shughuli za ardhi bila usimamizi wa wataalamu waliosajiliwa, hali inayochangia kupotea kwa uaminifu katika sekta hiyo.
Amesema ipo haja ya Serikali kuharakisha sheria ya udhibiti wa milki ili shughuli zote za udalali na uwekezaji wa ardhi zifanywe kwa kufuata taaluma, maadili na usimamizi wa kitaalamu.
“Tunahitaji mfumo utakaoweka uwajibikaji kwa kila anayejihusisha na shughuli za milki ili kulinda wananchi pamoja na wawekezaji,” amesema Yumba.
Aidha, amesema hata madalali wanaosajiliwa wanapaswa kufanya kazi chini ya wataalamu wa sekta hiyo ili kuongeza ufanisi na kuondoa migogoro inayotokana na biashara zisizo rasmi.
Kwa upande wake, Katibu wa chama hicho, Linda Msaki, alisema mkutano huo unajadili pia uanzishwaji wa mamlaka maalumu ya kusimamia sekta ya milki nchini ili kuongeza uwazi na kuimarisha usimamizi wa shughuli za uwekezaji wa ardhi na nyumba.
Mkutano huo umebeba kaulimbiu ya kujadili mbinu mbalimbali za uwekezaji wa pamoja katika sekta ya milki ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kufikia malengo ya maendeleo ya taifa ifikapo mwaka 2050.

More Stories
TAKUKURU Kinondoni yaainisha mafanikio Januari_ Machi 2016
Serikali yafikisha Umeme Katika Migodi 289 ya Wachimbaji Wadogo
Vipaumbele tisa bajeti Maliasili na Utalii