May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CHWs waimarishwa kuwabaini watoto wenye changamoto

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Magu

TAASISI ya Mwanangu Development Tanzania (MWADETA) imeendelea kuimarisha uwezo wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHWs),ili kuwabaini watoto wanaoishi kwa kufichwa nyumbani kutokana na changamoto mbalimbali za kiafya na ulemavu.

Akizungumza Mei 12,2026 katika mafunzo ya kuwajengea uelewa CHWs 25, kutoka Wilaya ya Magu mkoani Mwanza,yaliofanyika hospitali ya ya Wilaya hiyo,Mkurugenzi wa MWADETA Walter Miya,alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa programu iliyokwisha kufanyika katika wilaya za Nyamagana na Ilemela.

Ambayo yamelenga kuwajengea uwezo wa kuwabaini watoto wenye changamoto mbalimbali ikiwemo vichwa vikubwa, mgongo wazi na ulemavu mwingine unaowafanya kukosa huduma muhimu wakiwa nyumbani ili kupata huduma za afya,elimu na ustawi wa kijamii pamoja na kuondoa unyanyapaa.

Miya amesema tangu kuanza kwa utoaji wa elimu hiyo katika wilaya zilizotangulia, kumekuwa na mafanikio ambapo wahudumu hao wamefanikiwa kuwabaini watoto wengi waliokuwa wamefichwa ndani na kunyimwa huduma za afya, elimu na ustawi wa jamii.

“Tumeweka mfumo wa rufaa utakaowawezesha wahudumu hao kufikisha changamoto zinazoshindikana kutatuliwa ngazi ya kata kwa Maofisa wa wilaya husika. Kupitia mfumo huo, watoto wenye mahitaji maalum wataweza kupata huduma stahiki kwa wakati, huku taasisi hiyo ikitarajia kupata taarifa sahihi kutoka kwenye jamii kuhusu hali halisi ya watoto wenye changamoto katika Mkoa wa Mwanza na kuzifanyia kazi,”amesema Miya.

Kwa upande wake Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma Mkoa wa Mwanza ,Renard Mlyakado,amesema Mkoa huo kwa kushirikiana na MWADETA wanajitahidi kuwaibua watoto wenye changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili waweze kuwaibua watoto hao.

“Katika mkoa wetu tuna maeneo ambayo tunatumia kwa ajili ya matibabu ya watoto hao ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure na Rufaa ya Kanda Bugando.Mzazi mwenye mtoto anachangamoto hizo ili kupata huduma mapema,Mashirika haya yameelezwa kusaidia kuelimisha jamii pamoja na kuwaunganisha na vituo vya kutolea huduma pamoja n kupata huduma jumuishi baada ya kuwa wameisha pata matibabu,”amesema Mlyakado.

Naye Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Wilaya ya Magu, Joyce Sabora,amesema kwa sasa watoto wanaozaliwa na changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi kwa hospitali hiyo ipo kwa kiasi kidogo na wanapokutana na changamoto kama hiyo utoaji Rufaa ili mtoto huyo akapate matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.

“Tumekuwa tukiwaelimisha wanawake kwamba ni vizuri wakiwa wanajiandaa kupata ujauzito miezi miwili kabla watumie vidonge vya folic acid, changamoto wengine wanabeba ujauzito bila kujiju hivyo tunaendelea kutoa elimu pamoja na kuwahimiza wahudumu wa afya ngazi ya jamii kutoa elimu hiyo,kwani madini hayo kwa kiwango kikubwa ni kinga ya kuzuia mtoto kuzaliwa na mgongo wazi na kichwa kikubwa,”amesema Sabora.

Naye CWH kutoka Kata ya Isandula wilayani Magu,Stahamil Samwel,ambaye kupitia mafunzo hayo ameweza kumuibua mtoto mwenyewe ulemavu huku akisisitiza kuwa elimu walioipata itawawezesha kuwaibua watoto wengi zaidi wenye changamoto na kuhakikisha wanapata huduma stahiki.