May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndejembi akemea Wakandarasi wanaokwepa wazabuni

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),Lazaro Twange kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kumtafuta Mkandarasi anayekwepa kulipa madeni ya wafanyabiashara wa Wilaya ya Ngara waliotoa huduma ya vifaa wakati wa utekelezaji wa mradi wa umeme, ambapo baada ya kukamilika kwa mradi aliondoka bila kuwalipa hadi sasa.

Waziri Ndejembi ametoa maelekezo hayo Wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara waliokuwa wakitoa huduma ya vifaa kwa Mkandarasi Azhar Construction Company Limited wakati akitekeleza sehemu ya mradi wa umeme wa Rusumo, ambapo hadi sasa amekuwa akikwepa kulipa akidai bado anaidai TANESCO.

“Mkurugenzi Mtendaji kwa kufuatilia fuatilia, nimeambiwa kwamba Mkandarasi yule haidai TANESCO hata shilingi 10, ameshalipwa fedha zote”amesema Waziri Ndejembi.

Waziri Ndejembi ameelekeza kuwa Mkandarasi huyo akikwepa kulipa madeni hayo, asipewe kazi nyingine yoyote ndani ya TANESCO wala REA, kwani anachafua taswira ya Serikali kutokana na wananchi kufahamu kuwa alikuwa akitekeleza mradi unaosimamiwa na TANESCO.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Ngara,Dotto Bahemu amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ukamilishaji wa mradi wa umeme wa Rusumo, ambapo wananchi wa Wilaya ya Ngara walipata fursa na manufaa makubwa wakati wa utekelezaji wake.

Bahemu ameeleza kuwa Kampuni ya Azhar Construction Company Limited iliyotoa kazi kwa wafanyabiashara wa Wilaya ya Ngara, imekuwa ikiwazungusha na kukwepa kulipa madeni yenye jumla ya shilingi milioni 221 kwa huduma ya vifaa walizotoa wakati wa utekelezaji wa mradi huo.