HTM waeleza changamoto ya maji Korogwe
Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOline,Korogwe
MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM) imesema moja ya changamoto kwenye kutoa huduma ya maji kwenye Mji wa Korogwe ni uchakavu wa miundombinu ya maji.
Lakini pia, ukosefu wa miundombinu ya kusafisha na kuchuja maji (Water Treatment Plant), hivyo kufanya maji yanayozalishwa kutokuwa na ubora hasa nyakati za mvua.

Hayo yamesemwa Mei 6, 2026 na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HTM Robert Mtatiro kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Korogwe.
Kwenye taarifa yake iliyosomwa na Afisa Biashara wa HTM, Nar-dhwan Rashid, Mtatiro alisema changamoto nyingine ni uchakavu wa dira za maji, hivyo kuongeza upotevu wa maji na kupunguza mapato, na uchafuzi wa maji unaotokana na shughuli za kibinadamu zinazofanyika kwenye maeneo ya vyanzo vya maji, hususani uchimbaji wa madini katika chanzo cha Vuga- Nkozoi.

Mtatiro amesema mipango iliyopo ya kumaliza changamoto ya maji katika Mji wa Korogwe, na Mji Mdogo wa Mombo ni kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa maji pamoja na kuboresha miundombinu ya maji.
“Kuendelea kutumia vyanzo vilivyopo ili kuimarisha hali ya huduma ya maji ili kuhakikisha uendelevu wa huduma ya maji kwa wateja, kuendelea kutumia vyanzo vilivyopo ili kuimarisha hali ya huduma ya maji katika Mji wa Korogwe na Mombo, kuendelea kubadili dira za maji ambazo ufanisi wake umepungua katika maeneo ya Korogwe mjini, na kulinda vyanzo vya maji kwa kushirikiana na Ofisi ya Bodi ya Maji Bonde la Pangani,”amesema Mtatiro.

Mtatiro amesema kazi zilizotekelezwa katika kipindi cha mwezi Aprili, 2026 ni pamoja na kuziba mivujo katika maeneo mbalimbali ili kupunguza upotevu wa maji, kurudisha maunganisho ya maji kwa wateja baada ya kuhamisha miundombinu ya maji ili kupisha ujenzi wa barabara katika maeneo ya Manundu, Masuguru, TTC na Bagamoyo (Kijazi Road).
“Usafi wa vyanzo vya Mbeza na Mashindei, sambamba na usafi wa matenki pamoja na laini kuu za maji, usimamizi wa miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa ili kuhakikisha ubora na ufanisi, ukusanyaji wa Maduhuli yatokanayo na mauzo ya maji na maunganisho mapya kwa mwezi Machi, 2026 hadi Aprili, 2026″amesema Mtatiro.

Akichangia taarifa hiyo, Diwani wa Kata ya Manundu Rajabu Mzige amesema kasi ya kurudisha miundombinu ya maji mara baada ya kukatwa ama kuhamishwa kutokana na utengenezaji wa barabara bado ni ndogo, hivyo kasi iongezwe.
Akijibu hoja za madiwani ikiwemo maji kuwa machafu, Rashid alisema changamoto hiyo itaisha kwenye Mji wa Korogwe, hasa baada ya Mradi wa Miji 28 nchini kukamilika, kwani mradi huo kwa Mkoa wa Tanga kuna miji ya Korogwe, Handeni, Muheza na Pangani, na upo kamili ikiwemo mtambo wa kuchuja maji.

More Stories
Ujenzi wa Kituo cha Kupunguza Msukumo wa Mafuta Handeni wafikia asilimia 77
Wafugaji watakiwa kulinda ardhi yao
CHEVRON yaonesha nia ya kuwekeza Tanzania