Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOline,Korogwe
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Mji Korogwe (TD) mkoani Tanga Zahara Msangi amesema wamevunja Mkataba wa Mzabuni wa kuzoa taka ngumu kwenye halmashauri hiyo baada ya kukiuka Mkataba waliowekeana na kukubaliana..
Akijibu maswali ya papo kwa hapo kutoka kwa madiwani kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo Mei 6, 2026, Msangi alisema Mzabuni huyo ameshindwa kazi, kwani kwenye mkataba alisema atakuwa na magari mawili ya kuzoa taka, lakini kwenye utekelezaji limeonekana gari moja.

“Mkataba wetu na mtoa huduma ya kuzoa taka ilikuwa ni mwaka mmoja, lakini tulimpa miezi sita ya uangalizi ili kuona utendaji kazi wake, lakini baada ya kumfuatilia, tumeona ameshindwa kazi, sababu kwenye Mkataba alisema ana magari mawili, lakini kwenye utekelezaji wa kazi tumeona gari moja.
“Tunakwenda kuvunja Mkataba na yeye baada ya kuona ameshindwa kufanya kazi iliyokusudiwa ndani ya kata tano za Manundu, Majengo, Magunga, Kilole na Bagamoyo. Akimaliza muda wake wa uangalizi mwezi wa sita anaondoka, na sisi tayari tumeanza mchakato wa kumpata mtoa huduma mwingine, na ukiingia mwaka wa fedha mpya Julai Mosi, 2026/2027, tunataka tuwe na mtoa huduma mwingine”amesema Msangi.
Swali hilo liliulizwa na Diwani wa Kata ya Manundu, Rajabu Mzige, ambaye amesema kwa muda mrefu Mji wa Korogwe umekuwa mchafu, na bahati mbaya, wananchi wakiona mvua imenyesha, ndiyo wanachafua zaidi kwa kutupa taka ngumu kwenye mifereji, na uchafu huo kusambaa mji mzima. Hivyo kutaka kujua namna halmashauri itakavyoondoa changamoto hiyo.

Akifunga kikao cha Baraza la Madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Ali Mkwavingwa aliwataka watumishi kuwajibika kila mtu kwa nafasi yake ili kuleta ufanisi kwenye halmashauri hiyo, na kukiri mji wa Korogwe ni mchafu, hivyo maofisa afya waweze kupita kila kona ya mji huo ili kubaini vichaka vya uchafu, na watu wanaotupa taka hovyo, na hatua zichukuliwe dhidi yao.
“Ni kweli mji wetu ni mchafu, na mimi ni shahidi. Eneo la Posta pale kuna taasisi za fedha, kuna mitaro pale ukienda inatia aibu wakati ni usoni kabisa ya mji wetu. Kwa hiyo, mabibi afya na watendaji mliopo kwenye maeneo yetu, timizeni wajibu wenu. Tembeleeni na kuona watu wanaoweka vichaka na kushindwa kufanya usafi kipindi hiki cha mvua wafanye usafi ili mji wetu uendelee kuwa safi na salama”amesema Mkwavingwa.
Mkwavingwa amesema suala la chakula kwenye shule za msingi na sekondari ni la lazima, hivyo madiwani kama wenyeviti wa Kamati za Maendeleo ya Kata (WDC), wanatakiwa kulisimamia hilo ili kuhakikisha linafanikiwa kwa asilimia 100, kwani mtoto akila chakula shuleni anapata utulivu wa kusoma na kuelewa.

“Mimi naingiaga ofisini kikazi Jumanne na Alhamisi, lakini wakati mwingine situmii siku hizo kukaa ofisini, bali ninazitumia kutembelea shule mbalimbali, lengo ni kuwa na taarifa za kutosha ni namna gani halmashauri yetu inafanya kazi. Madiwani ndiyo wenyeviti wa Kamati za Maendeleo za Kata, suala la kula wanafunzi mashuleni ni suala la lazima sio ombi.
“Suala la kula watoto wetu mashuleni, sio suala la hiari ni la lazima, twendeni tukasimamie suala hilo kwenye shule zetu. Ni aibu kubwa kuona mtoto wa darasa la pili, darasa la tatu, ameshinda shuleni kuanzia saa moja asubuhi hadi saa tisa alasiri hajapata chochote, unatarajia mtoto huyu aje kuwa na uwezo gani wa kielimu katika kichwa chake. Ajenda ya kula iwe ya kudumu kwenye vikao vya kata zetu”amesema Mkwavingwa.

Mkwavingwa aliwaeleza Watendaji wa Kata ambao ni waalikwa kwenye Baraza la Madiwani, kuhakikisha wanawachukulia hatua wazazi ambao wanashindwa kuchangia sh. 500 ili watoto wao waweze kula shuleni.


More Stories
Prof.Mbawara:TMA yakamilisha ufungaji wa mitambo miwili ya uangazi wa hali ya hewa
PBPA yapongezwa kwa usimamizi wa upatikanaji wa Mafuta nchini
Ujenzi wa Kituo cha Kupunguza Msukumo wa Mafuta Handeni wafikia asilimia 77