Na Joyce Kasiki
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwaletea furaha na neema watumishi wa umma kupitia maboresho mbalimbali ya maslahi na mazingira ya kazi.
Kikwete amesema hayo wakati akizungumza na maafisa tawala na rasilimaliwatu katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Arusha International Conference Centre (AICC) mkoani Arusha.
Amesema maafisa hao wanapaswa kutekeleza wajibu wao kwa weledi na kuhakikisha watumishi wa umma wanapata huduma bora na mazingira yanayowapa motisha wa kufanya kazi kwa ufanisi.
“Tunapaswa kuendelea kuleta furaha kwa watumishi wa umma ili nao wakawe chanzo cha furaha na neema kwa wananchi wanaowahudumia kila siku,” amesema Kikwete
Aidha, alieleza kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha maslahi ya watumishi wa umma nchini, ikiwemo uamuzi wa hivi karibuni wa kupandisha madaraja watumishi 219,042, hatua aliyoiita ya kihistoria katika kuimarisha utumishi wa umma Tanzania.
Amesema maboresho hayo yamekwenda sambamba na ongezeko la mishahara ya watumishi wa umma kwa asilimia 35.1 mwaka 2025 pamoja na ongezeko la kima cha chini cha mishahara kwa sekta binafsi kwa asilimia 33.4 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Kwa mujibu wa Kikwete, sekta zitakazonufaika na maboresho hayo ni pamoja na afya, elimu, kilimo, mawasiliano, usafirishaji, nishati, viwanda, biashara, hoteli, michezo, uvuvi, baharini, madini na utamaduni.
Amesema mafanikio hayo yanaonesha kasi ya mageuzi ya kiutumishi chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, ambayo imeweka mbele ustawi wa watumishi wa umma pamoja na kuongeza ufanisi katika taasisi za serikali.

More Stories
Prof.Mbawara:TMA yakamilisha ufungaji wa mitambo miwili ya uangazi wa hali ya hewa
PBPA yapongezwa kwa usimamizi wa upatikanaji wa Mafuta nchini
Ujenzi wa Kituo cha Kupunguza Msukumo wa Mafuta Handeni wafikia asilimia 77