May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Fursa za Elimu ya Juu kupitia Mikopo,Udahili zaongezwa

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema Serikali imeendelea kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu nchini kupitia ongezeko la udahili wa wanafunzi vyuoni pamoja na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa shahada na stashahada.

Akizungumza Bungeni leo Mei 7,2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027,Prof.Mkenda amesema Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa elimu ya juu kwa kuratibu udahili wa wanafunzi katika vyuo mbalimbali nchini kwa mwaka wa masomo 2025/2026.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, jumla ya wanafunzi 170,916 waliomba kujiunga na elimu ya juu katika ngazi ya shahada ya kwanza, ambapo kati yao wanafunzi 159,010 sawa na asilimia 93 walidahiliwa.

“Idadi hiyo ni ongezeko la wanafunzi 21,193 ikilinganishwa na wanafunzi 137,817 waliodahiliwa mwaka wa masomo 2024/2025,” amesema Profesa Mkenda.

Ameeleza kuwa kati ya wanafunzi waliodahiliwa, wanawake ni 74,973 huku wanaume wakiwa 84,037, hatua ambayo amesema inaonesha kuendelea kuimarika kwa fursa za elimu ya juu nchini.

Aidha, amesema Serikali imeendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ili kuwawezesha wanafunzi wengi zaidi kufikia ndoto zao za kielimu.

Profesa Mkenda amesema katika mwaka wa fedha uliopita, jumla ya wanafunzi 284,487 walipatiwa mikopo ya elimu ya juu ikilinganishwa na wanafunzi 245,384 waliopata mikopo mwaka 2024/2025.

Amefafanua kuwa kati ya wanafunzi hao, wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopata mikopo ni 106,606, huku wanafunzi wa shahada ya kwanza wakiwa 94,451 na wa stashahada 11,844.

Vilevile, amesema wanafunzi wanaoendelea na masomo waliopata mikopo walifikia 177,881, hatua inayolenga kuhakikisha wanafunzi wanaendelea na masomo yao bila vikwazo vya kifedha.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imekusanya Shilingi bilioni 180.8 kutokana na marejesho ya mikopo iliyoiva.

Amesema kiasi hicho ni sawa na asilimia 82 ya lengo la ukusanyaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 220 kilichowekwa kwa mwaka huo wa fedha.

Profesa Mkenda amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya utoaji na urejeshaji wa mikopo ili kuhakikisha wanafunzi wengi zaidi wanapata fursa ya elimu ya juu na kuchangia maendeleo ya taifa kupitia taaluma mbalimbali.