


Na Mwandishi Wetu,Njombe
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) leo, Mei 1, 2026, imeungana na wafanyakazi wengine duniani kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), maadhimisho yaliyofanyika kitaifa mkoani Njombe.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye alikuwa mgeni rasmi. Katika hotuba yake, Rais Samia amewahimiza waajiri na waajiriwa kote nchini kuendeleza ushirikiano, kuaminiana, na kutanguliza maslahi ya taifa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira na ustawi wa wafanyakazi, huku akiwataka kuongeza bidii na ufanisi kazini. Aidha, alibainisha wazi kuwa Serikali inathamini mchango wa wafanyakazi na itaendelea kuwaunga mkono katika juhudi za maendeleo ya nchi.
Katika maadhimisho hayo, EWURA imewakilishwa na wafanyakazi wake bora kutoka idara na vitengo mbalimbali. Wafanyakazi hao walichaguliwa kwa kura za wenzao kwa kuzingatia vigezo muhimu kama vile utendaji uliotukuka, nidhamu ya kazi, ubunifu pamoja na kujituma kazini.
Wawakilishi hao walishiriki katika maandamano rasmi yaliyopita mbele ya mgeni rasmi, wakibeba mabango yenye ujumbe wa kuhamasisha mshikamano na uwajibikaji kazini.
Ushiriki wao umeonesha dhamira ya EWURA kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.

More Stories
Mchengerwa akabidhi boti za kuimarisha huduma za chanjo
Baobab wakutana na NBAA wapatiwa elimu ya Uhasibu
NMB yatwaa tuzo tano za Kitaifa za AOSH kwa mwaka wa Pili mfululizo