Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online -Kigoma
WANANCHI zaidi ya 20,000,kutoka Kata nne za Simbo,Kidahwe,Mongonya na Matendo,zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya kigoma,wameondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Hii ni baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha afya Simbo kilichogharimu zaidi ya sh.milioni 600 ambacho kimeanza kutoa huduma kwa wananchi.
Kituo hicho cha afya ambacho kina jengo la idara ya wagonjwa wa nje,maabara pamoja na wodi ya wazazi, ni mafanikio ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Afya inayoelekeza kila kata kuwa na kituo cha afya kitakachotoa huduma karibu na makazi ya wananchi.
Akizungumza na Timesmajira Online,Diwani wa Kata ya Simbo, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma,Neema Chikilanoza,alisema kata hiyo ni kubwa ikiwa na vijiji sita na ina wakazi wengi kuliko kata zote zilizopo ndani ya halmshauri hiyo.
Neema amesema,kabla ya kituo hicho kujengwa wananchi wa kata hiyo na Kata jirani,walilazimika kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 60 kufuata huduma za afya mjini, pia walitumia kiasi cha sh.100,000 hadi sh.150,000 kwa ajili ya usafiri wa kuwafikisha huko.
“Tunaishukuru Serikali kwa jitihada ambayo imefanya kwa kujenga kituo cha afya kwenye kata yetu,sasa wajawazito wanajifungulia hapo na tumeokoa vifo vya mama na mtoto kwa kiasi kikubwa.Kituo hiki kinategemewa na wananchi wa kata nne ikiwemo Simbo,Mongonya,Matendo na Kidahwe,”amesema Neema.
Mmoja wa wananchi wa Kata ya Simbo,James Sembese,amesema uwepo wa kituo hicho kimewasaidia wananchi kupata huduma nzuri kwa ukaribu, mazingira ni mazuri huku watoa huduma waliopo wakiwemo madaktari wanatoa huduma kwa wakati.
“Kituo hiki ni cha msingi kwetu wananchi, hivyo tunaomba Serikali ituongezee wahudumu wa afya ili waweze kufanya kazi kwa wakati na kutoa huduma bora zaidi,”amesema James.
Haya hivyo kituo cha afya cha Simbo ni miongoni mwa vituo vya afya ambavyo tayari vimejengwa kwenye kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma,kwa lengo la kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.
   Â

More Stories
TOSCI yawabana wauzaji holela wa mbegu
Kagera kunufaika na Mpango wa Afya Moja
Wiki usalama mahala pa kazi yafana Njombe