April 24, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaja na mageuzi makubwa sekta ya sheria

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma

SERIKALI kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imewasilisha mpango na bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ikiahidi mageuzi makubwa ya sekta ya sheria yenye lengo la kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati, kwa usawa na kwa ufanisi kwa Watanzania wote.

Akiwasilisha mpango huo bungeni jijini Dodoma leo Aprili 24,2026 , Waziri wa Katiba na Sheria amesema mwelekeo wa wizara hiyo umejengwa katika misingi ya kimkakati ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025 pamoja na Mpango wa Taifa wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV).

Amesema katika mwaka ujao wa fedha, wizara inalenga kuibadilisha sekta ya sheria kutoka kuwa ya utoaji huduma za kawaida hadi kuwa kichocheo cha maendeleo ya uchumi na uwekezaji nchini.

“Tunajenga sekta ya sheria inayotumia teknolojia, yenye ufanisi mkubwa na inayotoa haki kwa wakati. Lengo ni kuona sheria zinakuwa nguzo ya maendeleo ya Taifa,” amesema Waziri huyo.

Katika kufanikisha hilo, wizara imeainisha maeneo 15 ya kimkakati yatakayotekelezwa, ikiwa ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa haki hadi ngazi ya vijiji na kata, kuboresha msaada wa kisheria kupitia Kampeni ya Mama Samia (MSLAC), pamoja na kuanzisha mfumo wa ulinzi wa mashahidi na watoa taarifa za uhalifu.

Aidha, Serikali imepanga kuimarisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya sheria kwa kuanzisha mfumo wa kidigitali wa kitaifa wa msaada wa kisheria (e-Legal Aid) utakaorahisisha usajili na ufuatiliaji wa kesi pamoja na kuongeza uwazi na uwajibikaji.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo alibainisha kuwa Serikali itatekeleza awamu ya pili ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC II), akisisitiza kuwa mpango huo ni mageuzi ya msingi yatakayohakikisha kila Mtanzania anapata haki bila kujali hali yake ya kiuchumi au eneo analoishi.

“Huu siyo mpango wa kawaida, ni mabadiliko ya kimfumo yanayolenga kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma katika kupata haki,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa mpango huo, wizara pia itaweka mkazo katika kuimarisha taasisi za utawala bora, kuongeza ubora wa utungaji wa sheria, kuendeleza wataalam wa sekta ya sheria pamoja na kuboresha usimamizi wa mali za wadhamini na huduma za mirathi.

Serikali imeeleza kuwa utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kuongeza imani ya wananchi katika mfumo wa haki, kuboresha mazingira ya uwekezaji, kupunguza migogoro ya kisheria pamoja na kuimarisha uwajibikaji katika taasisi za umma.

Katika kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa, wizara imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi bilioni 774.7 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Waziri huyo aliliomba Bunge kuidhinisha bajeti hiyo, akisisitiza kuwa uwekezaji katika sekta ya sheria ni msingi muhimu wa kulinda maslahi ya Taifa na kuchochea maendeleo endelevu.

“Hatua hizi zitaiwezesha Tanzania kuwa na mfumo wa haki wa kisasa, unaotabirika na wenye ushindani kimataifa,” amesema.