November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa umeme wa pamoja Afrika Mashariki wafikia pazuri

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Kagera

UJENZI wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji, unaotekelezwa kwa ushirikiano baina ya nchi tatu wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Tanzania, Burundi na Rwanda katika Mto Kagera, umetajwa kuwa ni kielelezo bayana kinachoonesha uimara wa Mtangamano wa EAC.

Hayo yameelezwa wakati wa ziara ya siku nne ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Generali Wilbert Ibuge ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi ya mtangamano, inayounganisha nchi wanachama wa EAC, iliyofanyika katika Mikoa ya Kigoma na Kagera kuanzia Septemba 28 hadi Oktoba Mosi mwaka huu.

Katika ziara hiyo, Balozi Ibuge ametembelea ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 310 kutoka Nyakanazi-Kasulu hadi Manyovu, Mpaka na Burundi; Barabara ya kikanda (Tanzania/Uganda ya Bugene-Kasulo-Kumunazi kilomita 133, Kyaka-Mutukula (30 km)/Mutukula-Masaka kilomita 89.5.

Barabara hizo zinafanyiwa upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi; vituo vya kutoa huduma kwa pamoja mpakani (OSBPs) vya Kabanga (Tanzania na Burundi), Rusumo (Tanzania na Rwanda), Mutukula (Tanzania na Uganda) ambavyo ujenzi wake umekamilika na vinafanya kazi.

Balozi Ibuge Pia ametembelea eneo litakalojengwa OSBP ya Tanzania na Burundi katika mpaka wa Manyovu-Mugina, ambapo wataalamu wanaendelea na usanifu kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, kilichotengewa dola milioni 12 za Marekani na mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji katika Mto Kagera, unaojulikana kama Mradi wa Kikanda wa Kuzalisha Umeme wa Maji wa Rusumo.

Alipokuwa Rusumo, Balozi Ibuge ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi wa umeme ambao umefikia asilimia 67 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2022. Wahandisi wa mradi huo wamemweleza Balozi Ibuge kuwa ujenzi umegawanyika katika sehemu mbili, sehemu ya kwanza ni ujenzi wa Mtambo wa kuzalisha umeme ambao unagharimu dola za Marekani milioni 340.

Fedha hizo zimetolewa na Benki ya Dunia chini ya uratibu wa EAC na sehemu ya pili ni ujenzi wa njia za kusafirisha umeme ambao unafanywa na mashirika ya umeme ya kila nchi.

Benki ya Maendeleo ya Afrika imetoa dola za Marekani milioni 128.6 kwa ajili ya ujenzi wa njia hizo na taarifa iliyotolewa ni kwamba kila nchi imeanza kutekeleza ujenzi wa njia hizo.

Wahandisi hao wameeleza kuwa mtambo huo, utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa megawatti 80 ambapo kila nchi itapata mgawo wa megawatti 27. Wahandisi wamemuhakikishia Balozi Ibuge kuwa mradi huo, utakamilika kwa ubora unaotarajwa kwa kuwa wanapata ushirikiano wa kutosha kutoka kila nchi mshirika.

Balozi Ibuge kwenye miradi yote hiyo, amewasihi watumishi kutanguliza maslahi ya umma kwanza, kuliko maslahi yao binafsi.

Amesema miradi yote inalenga kuongeza kasi ya muingiliano wa watu, biashara ya bidhaa na huduma katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo asitokee hata mtu mmoja kwa maslahi yake akajaribu kuhujumu lengo hilo la EAC.