October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mchujo wachezaji timu ya Taifa wasogezwa mbele

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha mchezo wa Kabaddi Tanzania (TKSA) kimesogeza mbele mashindano ya Kabaddi kwa ajili ya kufanya mchujo huru wa wachezaji watakaounda timu ya Taifa (Open and fair trial selection at national level) .

Mchujo huo ambao utafanyika jijini Dar es Salaam utasimamiwa na Katibu na Kamati ya Ufundi na uteuzi huo utawahusu wale wote watakaopendekezwa na klabu zao.

Sababu za kuepeleka mbele tarehe ya kufanya mchujo huo ni baada ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kushauri chama hicho kushirikisha Mikoa mingi zaidi ishiriki ili kuongeza ushindani na kupata wachezaji bora watakaoweza kuwakilisha vizuri nchi kwenye mashindano ya kimataifa.

Mwenyekiti wa TKSA, Abdallah Nyoni ameuambia Mtandao huu kuwa, baada ya kuwasiliana na BMT waliwashauri kuongeza idadi ya Mikoa ili kuongeza ushindani zaidi.

Amesema, pia waliwaambia waangalie mfumo unaotumika Zanzibar na endapo ushindani utakuwa mkubwa basi nao washiriki kama nchi katika mashindano hayo na ikiwa watakuwa kawaida basi watawakilisha kama Mkoa.

“Tayari kuna vijana wetu wapo Zanzibar ambao wamekwenda kushughulikia jambo hilo na pia tunaendelea na programu zetu ndani ya mikoa mbalimbali ikiwemo Mwanza, Shinyanga, Mtwara, Arusha, Tanga, Mbeya ili kuzalisha wachezaji wenye ubora ambao watakuja kushindania kuingia katika kikosi cha timu ya Taifa,” amesema Nyoni.

Kufanyika kwa mchujo huo kutakuwa ni mwendelezo wa maandalizi kuelekea mashindano ya Kabaddi ya Afrika ambayo Tanzania atakuwa mwenyeji.

Katika mashindano hayo ya Afrika, Tanzania itawakilishwa na timu ya wanaume na wanawake pia zipo timu kutoka nchini Kenya, Cameroon, Egypt, Mauritius, Sirra Leone, Uganda, Afrika Kusini, Nigeria na Zimbabwe.

Lakini timu za Uingereza, Malaysia, Taiwan, Iraq na India zikionesha nia ya kuja kama waalikwa ingawa ushiriki wao utategemea maamuzi ya bodi ya Kabaddi Afrika (Africa Kabaddi Federation na World Kabaddi).

Kwa mujibu wa kalenda hiyo, mwezi ujao chama hicho kitaanza kuandaa tathimini na ripoti ya makusanyo ya pesa za kuendesha
mashindano pamoja na kupitia bajeti husika na kuwasafirisha wachezaji wataokwenda kuunga na timu zao za kulipwa nchini India kushiriki ligi ya ‘IIPKL’

Pia wataanza kushughulika vibali vya kuingia nchi kwa wachezaji wa kigeni, kupokea majina ya mwisho kwa wachezaji kwa timu shiriki pamoja na babadiliko ya majina ya wachezaji, viongozi yakiambatana na pasi zao za kusafiria kabla na si chini ya Novemba 30.

Novemba watapokea walimu wa Kabaddi kutoka nchini India
ili kuanza kwa kambi ya timu ya Taifa ya Kabaddi ambapo pia watafanya tathimini ya maandalizi ya mashindano ya Afrika ikiwa pamoja na kuandaa miundombinu ya mashindano (hotel kwa timu, viwanja, chakula na usafiri pamoja na kufanya semina elekezi kwa wanahabari wa Tanzania juu ya kuripoti mchezo wa kabaddi, sheria na kanuni nyingine.

Desemba 8 na 9, 2020 watapokea timu ya wakaguzi na maafisa wa ufundi pamoja na wanahabari toka nje watakaoambatana na maofisa wakuu wa World Kabaddi, Africa Kabaddi Federation na NKIF na Desemba 10 timu zitaanza kuwasili kwa ajili ya mashindano yatakayoanza tarehe 11 hadi 13.