April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waumini wakumbushwa nafasi ya Yesu

*Huku wakisisitizwa kudumisha haki na kuombea amani katika jamii na taifa

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza

WAUMINI wa Kikristo wamehimizwa kutafakari na kuyaishi mambo matatu muhimu wanapokaribia kumaliza kipindi cha Kwaresma, ikiwemo kumfanya Yesu Kristo kuwa mtawala wa maisha yao, kumtambua kama Mwokozi, pamoja na kuombea amani katika familia, jamii, taifa na nchi jirani.

Wito huo umetolewa Machi 29, 2026 na Mchungaji Emmanuel Muhangwa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ushirika wa Makedonia Mjimwema, Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, wakati wa ibada ya Sikukuu ya Matawi (Jumapili ya Mitende) iliyofanyika kanisani hapo.

Amesema siku hiyo huashiria mwanzo wa Juma Takatifu, kipindi ambacho Wakristo hukumbuka mateso ya Bwana Yesu Kristo.

Akihubiri, Mchungaji Muhangwa aliwataka waumini kutafakari mafundisho matatu makuu, akianzia na kumkaribisha Yesu Kristo kuwa mtawala wa maisha yao.

Amefafanua kuwa kwa mujibu wa Injili ya Mathayo 21:1–11, Wayahudi walimlaki Yesu kwa shangwe, wakitandaza matawi na kuacha shughuli zao, ishara ya kumpa nafasi ya kutawala maisha yao.

“Sisi kama Wakristo tunapaswa kujifunza kutandaza maisha yetu ili Yesu Kristo atawale. Akitawala maisha yetu, tutakuwa na jamii yenye hofu ya Mungu na kuacha matendo maovu,”amesema Mchungaji Muhangwa.

Aidha,amewahimiza waumini kuomba wokovu wa Yesu Kristo utawale maisha yao, akirejea Mathayo 21:9 inayosema, “Hosana Mwana wa Daudi, amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana,” akibainisha kuwa “Hosana” lina maana ya “okoa sasa”.

Ameongeza kuwa Wakristo wanapaswa kumwomba Yesu awaokoe dhidi ya changamoto mbalimbali zinazoikumba jamii, ikiwemo rushwa na ufisadi vinavyokwamisha maendeleo ya taifa na kanisa.

Katika hatua nyingine,amesisitiza umuhimu wa kuombea amani, akieleza kuwa Yesu Kristo aliingia Yerusalemu akiwa amepanda punda, ishara ya unyenyekevu na amani, tofauti na farasi ambaye huashiria vita.

“Kwa tendo hilo, Yesu anajitambulisha kuwa Mfalme wa amani, hivyo tunapaswa kumwomba atawale mioyo yetu, familia, jamii na taifa kwa amani,”amesisitiza Mchungaji Muhangwa.

Pia amesema, amani ni msingi muhimu wa maisha ya mwanadamu na maendeleo ya jamii, kwani inapokosekana utendaji kazi hudhoofika na hata uchumi kuyumba kutokana na watu kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Akizungumzia haki,amesema haki na amani ni mapacha, akisisitiza kuwa vinapaswa kuanzia nyumbani, jamii, kanisani na serikalini, ili kila mmoja atekeleze wajibu wake kulingana na mapenzi ya Mungu.