Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma
MKURUGENZI wa Shirika la Vijana wa Tanzania kwa Ujenzi wa Taifa (TAYNACO) Masasila Kadoke amezindua rasmi Sgirika hilo kwa lengo la kuongeza kasi ya matumaini kwa vijana, kuimarisha mshikamano wao na kujenga uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Kodoke alisema kuanzishwa kwa shirika hilo kunatokana na uhitaji wa dhati wa kuwa na jukwaa la kati litakalowaunganisha vijana, kusikiliza changamoto zao na kutoa suluhisho la vitendo bila kujikita katika misingi ya upande wowote wa kisiasa.
Alisema TAYNACO inalenga kumjenga kijana imara kiuchumi, kiakili na kimaadili, kwa kuamini kuwa kijana imara ndiye msingi wa Tanzania imara. Kaulimbiu ya shirika hilo ni “Kijana Imara, Tanzania Imara.”alisema Kadoke
Katika kufanikisha malengo yake, Kodoke alibainisha kuwa TAYNACO imejipanga kutekeleza programu na mifumo mbalimbali, ikiwemo mfumo wa kuunganisha vijana na fursa utakaokuwa daraja kati ya vijana na fursa zilizopo nchini.
“Kupitia mfumo huu, vijana wataweza kupata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu ajira, mafunzo, mikopo, ubunifu na uwekezaji,pia utarahisisha upatikanaji wa taarifa kwa njia za kidijitali ili kuhakikisha kijana wa kawaida, bila kujali alipo, anapata nafasi ya kuona na kuzifikia fursa zinazomzunguka,” alisema.
Aliongeza kuwa lengo la mfumo huo ni kumtoa kijana katika hali ya kusubiri bahati na kumweka katika nafasi ya kuchukua hatua.
Kuhusu programu ya vijana wenye ujuzi, Kodoke alisema inalenga kubadili ujuzi kuwa matokeo halisi ya kiuchumi kwa kuwatambua vijana wenye ujuzi mbalimbali kama vile ufundi, teknolojia, ubunifu na biashara ndogondogo, na kuwaunganisha katika mifumo ya kazi na miradi.
Aidha, kwa vijana wasiokuwa na ujuzi, alisema TAYNACO itatoa fursa za mafunzo ya vitendo kwa kushirikiana na wataalamu na wadau mbalimbali, ili kuhakikisha kila kijana anakuwa na uwezo wa kujitegemea katika uchumi wa Taifa.
Mipango mingine iliyotajwa ni pamoja na kuanzishwa kwa mfuko wa kukuza ubunifu wa vijana, jukwaa la kusikiliza vijana pamoja na mpango wa kitaifa wa kuimarisha matumaini na ushiriki wa vijana.
Kwa upande mwingine, shirika hilo limeahidi kushirikiana na Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ili kuhakikisha vijana wanarejea na kuishi misingi aliyoiamini Baba wa Taifa, ikiwemo uadilifu katika maisha na uongozi, uzalendo na upendo kwa Taifa, haki na usawa kwa kila Mtanzania, amani na mshikamano wa kitaifa pamoja na kujitegemea na kufanya kazi kwa bidii.
Naye Katibu Mkuu wa TAYNACO, Sadick Augustino, alisema shirika hilo litahakikisha linakuwa sauti ya vijana nchini kwa kuwasikiliza na kuwashirikisha kikamilifu katika mchakato wa maendeleo ya Taifa.

More Stories
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini
REA imeleta mageuzi sekta ya nishati