Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
MKUU wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza,Amiri Mkalipa,amewatoa hofu wananchi wa wilaya hiyo juu ya chanjo ya polio inayotarajiwa kutolewa kwa watoto Machi 24 hadi 27,2026 huku akiwataka kuondoa dhana potofu juu ya chanjo hiyo.
Ambapo Halmashsuri ya Manispaa ya Ilemela inatarajia kutoa chanjo ya polio kwa watoto 146,956 wenye umri chini ya ya miaka 10.

Chanjo hiyo inatolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kampeni maalumu ya chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka 10,katika mikoa saba ikiwemo Mwanza,Geita,Tabora,Simiyu, Shinyanga, Singida na Mara.
Akifungua mafunzo ya kampeni ya polio ya matone kwa Kamati ya Afya ya Msingi (PHC), yaliofanyika Machi 19,2026,Mkalipa amesema kuwa chanjo ya polio ya matone ni salama na imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na kuidhinishwa na Wizara ya Afya.
Mkalipa amesema zoezi hilo litafanyika nyumba kwa nyumba na mtoto kwa mtoto na mahali popote ambapo mtoto anaweza kuwepo atafikiwa na wataalamu.
Hivyo ametoa wito kwa viongozi wa dini, na viongozi waandamizi kutoa elimu sahihi kwa jamii ili kuondoa imani potofu kuhusu chanjo ya polio na kuhakikisha watoto wote wenye umri husika wanapatiwa chanjo hiyo kwani ugonjwa wa polio ni hatari.
“Viongozi wa dini mtupaazishie sauti kwa waumini wenu juu ya chanjo hii itakapoanza na kuondoa dhana potofu kwamba mtoto akichanja anaweza asizae ama apoteze nguvu za kiume,” amesema Mkalipa.

Kwa upande wake Mratibu wa chanjo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Shamte Almasi,amesema kuwa hadi sasa, hakuna mtoto aliyethibitika kuugua ugonjwa wa polio nchini Tanzania.
Hivyo kampeni hiyo maalum inafanyika kama hatua za tahadhari ya mapema ya kuwakinga watoto na jamii kwa ujumla wasipate maambukizi ya ugonjwa wa polio.
Hata hivyo kampeni hiyo inalenga kuimarisha kinga-jamii dhidi ya ugonjwa wa polio na kuzuia uwezekano wa maambukizi ya virusi kutoka kwenye mazingira kwenda kwa binadamu.


More Stories
Silinde azindua baraza la sita la Wafanyakazi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini