*Mkalipa, asisitiza fedha kuelekezwa kwenye miradi husika na kurejesha kwa wakati
*Hatua kuchukuliwa kwa watakaoshindwa kurejesha
Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026,imetoa mkopo wa shilingi milioni 463, kwa vikundi 41 vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu,kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani.
Akizungumza Machi 18,2026,katika hafla ya kukabidhi hundi ya mkopo huo kwa vikundi hivyo,iliofanyika katika halmashauri hiyo,Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Amiri Mkalipa,alivitaka vikundi hivyo kuzingatia matumizi sahihi ya fedha hizo pamoja na kurejesha kwa wakati ili wengine waweze kunufaika, kuhakikisha fedha hizo zinaelekezwa kwenye miradi husika huku vijana kutotumia mkopo huo kuongeza mke mpya.
“Kila Kata ina Ofisa Maendeleo ambao kila mmoja alipewa pikipiki,hatutaki fedha hizi zipotee.Fedha ya kikundi ikipotea tunaanza na Ofisa Maendeleo wa Kata husika,tutamchukulia hatua madhubuti na za kinidhamu kisha tutakuja kwenye kikundi,”alisema Mkalipa.

Mkalipa, aliwasisitiza kuwa mtu akipewa imani na Serikali yakukopeshwa aoneshe uaminifu huo kwa kurejesha kwani yapo yapo mamia ya vikundi vimeomba mkopo navimekosa.
“Mshukuru Mungu wa kupata na atakayechezea fedha hizi lazima tutamchukulia hatua kali na madhubuti tutamsokota barabara.Nayaweza mambo yote katika yeye anitiyae nguvu,na hili la kuchukua hatua naliweza,ni jukumu langu nimeaminiwa,na nimelifanya siyo mara moja,siyo mara mbili,siyo mara tatu.Na wewe haitakuwa wa kwanza kukuchukulia hatua ukianza kupepesa macho katika kulipa,”alisema Mkalipa.
Aliwasihi vijana kutotumia fedha hizo kufanya starehe na badala yake wazingatie marejesho kwani bila kufanya hivyo watakutana na pilato huku akisisitiza kuwa vipo vikundi ambavyo havikurudisha mkopo tayari wameanza kuvisokota na kuvipeleka mahakamani na lazima watalipa.
“Fedha hizi ukurejesha kwa wakati inafanya wanawake na vijana wengine wakope na Serikali haikimbiliki.Mikopo yetu tumeondoa riba ukikopa milioni 20 utarejesha hiyo hiyo,lakini taasisi nyingine za kifedha ukikopa milioni 10 unarejesha na riba ndogo si pungufu ya asilimia 10,”alisema Mkalipa.

Awali Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Yusuph Omollo,alisema halmshauri hiyo ilitoa tangazo la utengaji wa fedha kiasi cha shilingi milioni 625 kwa kipindi cha robo ya tatu Januari hadi Machi 2025/2026,hadi kufikia Desemba 2025 ilipokea jumla ya maombi ya mkopo ya vikundi 181 yenye thamani ya shilingi zaidi ya bilioni 5.366. yaliyoombwa kupitia mfumo wa Wezesha Portal.
Kati ya hivyo vikundi vya wanawake vilikuwa 97 vyenye thamani ya zaidi ya bilioni 3.662,vijana vikundi 75 vyenye thamani ya zaidi ya bilioni 1.653 na watu wenye ulemavu 9 vyenye thamani ya milioni 50.
Yusuph alisema,baada ya kamati ya uhakiki wa mikopo kufanya uhakiki wa vikundi iliweza kushauri na mwisho kamati ya menejimenti iliridhia na kuidhinisha kiasi cha milioni 463 kwa vikundi 41,kati ya hivyo vikundi 20 vya wanawake vinapata milioni 230,vijana vikundi 15 vinapata milioni 192 huku sita watu wenye ulemavu ambao wanapata kiasi cha shilingi milioni 4.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Goodluck Lukandiza,alisema,
“Tunaamini mikopo hii itaenda kuinua au kuboresha maisha pamoja na shughuli za wanufaika walioomba.Rai yetu mikopo hii iende kutumika kwa ajili ya miradi walioombea na haitolewi bure hivyo wanapaswa kurejesha ili na wengine waweze kupata hivyo hatutegemea kesho na kesho kutwa kuingia katika changamoto ambayo hatukuitegemea kisa tu hawajarejesha,”.
Mmoja wa wanufaika wa mikopo hiyoJane John, alisema mikopo hiyo itawawezesha kujikwamua kiuchumi pamoja na kuajiri wengine kupitia miradi walioanzisha. huku akisisitiza kuwa watarejesha kwa uaminifu ili na wengine waweze kukopa.




More Stories
TCB yazinduz kampeni ya kuchochea uchumi ,kuwezesha ndoto za Watanzania
77 mbaroni tuhuma za kuhujumu miundombinu ya reli
Mnzava awataka wananchi Muheza kujiepusha na migogoro ya ardhi