March 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge Ardhi yatoa maelekezo Korogwe DC

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOline,Korogwe

KAMATI ya Kudumu ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii imeiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga watakapouza viwanja awamu ya pili, kipaumbele kiwe kwa wananchi wa Kata ya Hale.

Na hiyo inafuatia malalamiko yaliyotolewa na wananchi wa kata hiyo kuwa, awamu ya kwanza ya uuzaji wa viwanja 900, waliuziwa wananchi kutoka nje ya kata hiyo, na hiyo ilitokana na changamoto mbalimbali ikiwemo viwanja hivyo kuuzwa kwa njia ya mtandao kupitia malipo ya Serikali ya Mfumo wa Tausi, ambapo wananchi wa kawaida walishindwa kuijua njia hiyo.

“Makamu Mwenyekiti Kamati ya Bunge, Ardhi, Mary Masanja, akitoa maelekezo kwa Korogwe DC.”

Maagizo hayo yaliyotolewa Machi 16, 2026, na kusomwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mary Masanja. Ni baada ya Wajumbe wa Kamati hiyo kufika kwenye Mradi wa Viwanja uliopo Kijiji cha Makinyumbi Stesheni, na Kijiji cha Makinyumbi Mwembeni.

Baadhi ya maagizo mengine ni kwamba halmashauri watakapokuwa wanauza viwanja 1,900 kwa awamu ya pili, Wizara ya Ardhi itatuma mwakilishi wake ili kuja kusimamia zoezi hilo, kuona ugawaji huo unazingatia wenyeji wa Kata ya Hale, na hususani wale wa vijiji vya Makinyumbi Stesheni na Makinyumbi Mwembeni ambao ndiyo walikuwa waathirika wa kufa kwa mashamba ya mkonge.

“Kwenye hivi viwanja ambavyo havijapandishwa kwenye Mfumo, na vingine vitakavyopimwa kwenye shamba hili usimamizi uwe chini ya Wizara ya Ardhi. Watakapopandisha kwenye viwanja hivi vilivyobaki, ugawaji, wizara yenyewe itatuma mwakilishi hapa kushirikiana na watumishi wa halmashauri kuhakikisha ugawaji uwe ni wa haki, na wenyeji wawe kipaumbele.

“Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Goodluck Mwangomango (katikati) akijibu hoja za Wajumbe.”

“Na hili ninalielekeza sababu kumekuwa na malalamiko makubwa sana kwa upande wa wananchi wenyeji. Kwa hiyo tunaielekeza wizara, na wizara inashirikiana na halmashauri kuhakikisha wanatafuta namna iliyo bora bila kuathiri sheria zilizopo, bila kuathiri mipango iliyopo, lakini ifanyike namna ya kuwafanya hawa wenyeji kupata haki ya msingi. Kama viongozi wao walipigania eneo hili likafutwa (umiliki wa shamba la mkonge), cha kwanza tulitakiwa tuwaone hawa wenyeji, na baadae kama mnauza, basi mnauzia wengine” alisema Masanja.

Masanja alisema wanaamini eneo hilo viwanja vyake ni vipya na vimepimwa, hivyo viwanja hivyo wamewataka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na halmashauri, viwanja hivyo havitasababisha mgogoro wa aina yeyote, na kama kuna mtumishi wa halmashauri atasababisha mgogoro na amehamishwa, atafuatwa huko huko ili aje kujibu hoja zake.

Masanja pia kwa niaba ya Wajumbe, wameitaka halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya kutengeneza barabara kwenye viwanja hivyo vipya, kwani pamoja na kuwa vitavutia wanunuaji, lakini pia vitasaidia kuvijua viwanja vyao kwa urahisi, na wale wanaotaka kupeleka vifaa vya ujenzi iwe rahisi kufika.

“Mwenyekiti wa Kijiji cha Makinyumbi Stesheni, Simon Stelio akitoa maelezo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii.”

Awali, akijibu hoja za Wajumbe wa Kamati, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Goodluck Mwangomango alisema mradi wa kuuza viwanja una viwanja 5,000, na hadi sasa wameuza viwanja 900 awamu ya kwanza, na wamepata sh. 1,042,000,000, ambapo kati ya fedha hizo, sh. milioni 800 wamepeleka kwenye shughuli za maendeleo ikiwemo afya, ambapo ukarabati wa Zahanati ya Makinyumbi Mwembeni ambayo majengo yake ilikuwa kambi ya watengeneza barabara. Pia kuna elimu, na ukopeshaji wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Mwangomango alisema uuzaji wa viwanja awamu ya pili utahusisha viwanja 1,900, ambavyo kipaumbele kitakuwa wananchi wa Kata ya Hale ambao kwenye awamu ya kwanza wenyeji wa Hale hawakupata, na hiyo ni kutokana na njia iliyotumika ya malipo ya Serikali mtandaoni kupitia Mfumo wa Tausi.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Makinyumbi Stesheni, Simon Stelio aliwaeleza Wajumbe wa Kamati kuwa shida yao ni viwwnja, kwani wananchi waliobaki kwenye mabaki ya nyumba zilizokuwa kambi za mkonge, wameongezeka, na wanahitaji wajenge nyumba bora. Hivyo, wanaomba wagawiwe viwanja bila kutumia Mfumo wa Tausi, kwani wananchi hawana uwezo wa kuombea kupitia mfumo huo, na badala yake viwanja vigawiwe kwa kushirikisha viongozi wa vijiji na kata.

“Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Kaspar Mmuya akizungumza alipofika Kijiji cha Makinyumbi Stesheni.”

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii inayoongozwa na Mbunge wa Korogwe Vijijini TimotheoMnzava, ilifika Wilaya ya Korogwe ili kukagua miradi ya maendeleo, ambapo kwa upande wa Serikali, pia alikuwepo Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Kaspar Mmuya, na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga.

“Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, na na Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini Timotheo Mnzava akizungumza kwenye Kijiji cha Makinyumbi Stesheni.”
“Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii wakiwa ukumbini mjini Korogwe kusubiri Wasilisho la Mradi wa Viwanja Kata ya Hale.”
“Makamu Mwenyekiti, Kamati ya Kudumu ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii Mary Masanja (kushoto) akisalimiana na Afisa Tarafa ya Korogwe, Gloria Sanga. Ni baada ya kufika Ofisi ya DC Korogwe.”