Na Moses Ng’wat, TimesmajiraOline,Songwe.
ASKOFU wa Kanisa la The House of Prayer International Ministry, Kanda ya Songwe na muimbaji wa nyimbo za injili, Sarah Wega , amefariki dunia baada ya kupata ajali ya kugongwa na lori iliyotokea Machi 16, 2026 katika eneo la Chapwa, Wilaya ya Momba mkoani Songwe.
Taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa Askofu Sara alipata ajali akiwa kwenye usafiri wa bodaboda akielekea kijiji cha Chiwezi kwa ajili ya kumtembelea ndugu yake anayesimamia mashamba ambaye naye anaripotiwa kuwa alipata ajali akiwa shambani.
Katika ajali hiyo, dereva wa bodaboda (jina halijafahamika) alifariki papo hapo, huku Askofu Sara akifariki dunia baadaye alipokuwa akipatiwa matibabu hospitali katika hospital ya rufaa ya mkoa wa songwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Agustino Senga, hakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo licha ya juhudi za waandishi wa habari kufika ofisini kwake, ambapo walielezwa kuwa yupo kwenye kikao cha mtandaoni na hata alipopigiwa simu mara kadhaa hakupokea.
Akizungumza nyumbani
kwa marehemu ambako shughuli za maombolezo zinaendelea, kaka wa marehemu, Michael Wega, amesema alipokea taarifa za ajali hiyo majira ya saa 3:00 usiku wa Machi 16, 2026.
“Nilipata taarifa kuwa mdogo wangu amepata ajali eneo la Chapwa akiwa kwenye bodaboda baada ya kugongwa na lori. Dereva wa bodaboda alifariki papo hapo, lakini mdogo wangu alifariki baada ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, kufuatia kupatiwa matibabu ya awali katika Kituo cha Afya Chapwa,” ameeleza.
Kwa upande wake, msemaji wa kanisa hilo, Gervasi Mwanyula, ambaye pia ni msaidizi wa Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Furaha Mwakabenga, amesema kanisa limepokea tukio hilo kwa masikitiko makubwa.
Amesema marehemu, mbali na kuwa kiongozi wa kiroho, pia alikuwa akihudumu kupitia nyimbo za injili na kugusa maisha ya waumini wengi.
Aidha, amebainisha kuwa shughuli za maombolezo zinaendelea nyumbani kwa marehemu katika eneo la Vikandamoyoni, mjini Vwawa, Wilaya ya Mbozi, huku mazishi yakitarajiwa kufanyika Machi 19, 2026 katika madhabahu ya Sarah Wega kanisa la Ilolo, alilokuwa akiliongoza.

More Stories
EWURA, WRBWB ,TFS wapanda miti kuadhimisha wiki ya Maji Duniani
Mchechu azitaka kampuni ambazo Serikali ina hisa chache kukumbatia uongozi wa kimkakati
Majiko ya umeme yaleta mapinduzi shule sita za msingi Tabora