March 15, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Zanzibar aipongeza Yas, Mixx mageuzi ya kidigitali

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameipongeza kampuni ya Yas pamoja na Mixx kwa mchango wao endelevu katika mageuzi ya kidijitali na ukuaji wa uchumi visiwani humo.

Pongezi hizo zilitolewa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Hamza Hassan Juma wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na kampuni hiyo visiwani Zanzibar juzi.

Juma meeleza kuwa, uwekezaji wa kampuni hiyo katika upanuzi wa mtandao, huduma za kifedha kidijitali na programu za kijamii zinaunga mkono moja kwa moja ajenda pana ya Serikali ya kujenga uchumi wa kisasa na jumuishi unaotegemea teknolojia.

“Serikali inathamini mchango wa wadau wa sekta binafsi wanaounga mkono dira yetu ya taifa ya Zanzibar yenye nguvu ya kidijitali,” amesema, akisisitiza nafasi ya Yas katika kuimarisha mawasiliano na kupanua upatikanaji wa huduma za kidijitali visiwani humo.

Hafla hiyo ya futari iliambatana na zoezi lingine la kijamii ambapo Kampuni ilitoa bima ya afya kwa watoto 200 kutoka jamii zilizo katika mazingira magumu Zanzibar.

Mpango ambao ulipokelewa kwa mikono miwili na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Abeida Rashid Abdallah, amesema:

“Kwa niaba ya Wizara, tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Yas Tanzania kwa mchango huu wenye manufaa makubwa. Kwa kutoa bima ya afya kwa watoto 200 waishio kwenye mazingira magumu, kunawapa fursa ya kupata huduma muhimu za matibabu, afya njema na kujiamini.

“Mpango huU unaonyesha dhamira pana si tu kuunganisha jamii zetu kidijitali, bali pia kulinda ustawi na heshima yao,” amesema.

Viongozi wa Serikali, wawakilishi wa taasisi mbalimbali, wadau na wateja wamehudhuria hafla hiyo, ambayo pia ilitumika kutathmini maendeleo yaliyopatikana tangu kuzinduliwa kwa chapa za Yas na Mixx nchini Tanzania mwaka mmoja uliopita.

Katika hotuba yake kuu, Afisa Mtendaji Mkuu wa Yas Tanzania, Pierre Canton-Bacara, amegusia dhamira ya kampuni hiyo katika kuimarisha uwepo wake Zanzibar kupitia miundombinu ya kidijitali, ujumuishaji wa kifedha na programu za kijamii.

Amebainisha kuwa, Yas sasa inaendesha mtandao mpana na wenye kasi zaidi wa 4G na 5G nchini uliothibitishwa na Ookla kwa mwaka wa tatu mfululizo hatua inayowawezesha Wazanzibari kupata kwa urahisi huduma za kidijitali, elimu, biashara na masoko ya kimataifa.

“Zanzibar ina nafasi ya kipekee katika safari yetu ya ukuaji. Kazi yetu hapa haiishii kwenye mawasiliano tu; inalenga pia kuunda fursa kwa watu binafsi, kaya na biashara,” amesema Bacara.

Ameongeza kuwa, “Tunaendelea kujizatiti kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wadau wote ili kuunga mkono ukuaji endelevu wa uchumi wa kidijitali Zanzibar.”

Ametaja mafanikio kadhaa yaliyopatikana kwa ushirikiano na Serikali, ikiwa ni pamoja na:•

Ujenzi unaoendelea wa minara mipya ya mawasiliano kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ili kupanua huduma katika maeneo ambayo hayajafikiwa.•

Mipango ya kusambaza mkongo wa mawasiliano (fibre) ili kuunganisha nyumba, taasisi na biashara visiwani Zanzibar.

“Uwekaji wa mifumo ya kidijitali katika huduma muhimu za umma kupitia Mixx Super App ikiwemo TUKUZA, malipo ya ada za shule kupitia Lipa Ada, malipo ya maegesho, huduma za mapato za ZRA na malipo ya matibabu ya ZHC.•

Mifumo ya malipo ya kidijitali kwa wakulima zaidi ya 10,000 wa karafuu kwa kushirikiana na ZSTC, ambapo zaidi ya Shilingi bilioni 48 tayari zimelipwa kupitia Mixx, pamoja na utoaji wa bima ya afya yenye thamani ya Shilingi milioni 350 chini ya mpango wa Afya Mkulima na upandaji wa miche 25,000 ya mikarafuu.

Zaidi ya Wazanzibari 25,000 kwa sasa wanapata kipato kupitia Yas na Mixx kama mawakala, watoa huduma na wajasiriamali wa kidijitali.

Aidha, Yas imetoa msaada katika sekta za elimu na afya kwa kutoa intaneti bure kwa shule 52 hatua inayowanufaisha zaidi ya wanafunzi 31,000 pamoja na kuendesha kambi za matibabu ya macho bila malipo ambazo zimewahudumia maelfu ya wananchi kwa ushauri wa kitaalamu na matibabu.

Mtendaji Mkuu huyo amehitimisha kwa kuwashukuru wadau kwa imani na ushirikiano wao.

“Tunajivunia imani tuliyopewa na wananchi pamoja na Serikali ya Zanzibar.

” Ushirikiano huu unatuhamasisha kuendelea kuwekeza, kubuni na kuboresha huduma tunazotoa,” amesema,

Ametoa pia, salamu za heri kwa siku zilizobaki za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na maandalizi ya Sikukuu ya Eid.