March 15, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas yafuturisha wakazi wa Mbagala

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online

KAMPUNI ya Yas Tanzania, imeshiriki futari ya pamoja na wateja, viongozi wa dini na wakazi wa Mbagala.

Hiyo ikiwa ni sehemu ya utamaduni wake wa kuungana na jamii katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Hafla hiyo imeongozwa na Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Kaskazini,  Robert Kasulwa.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo hivi karibuni, Kasulwa amesema futari ya pamoja ni ishara ya kuthamini uhusiano uliopo kati ya kampuni na wananchi wanaotumia huduma zake, hususan katika maeneo ya mijini na pembezoni ambako mawasiliano ni sehemu muhimu ya maisha ya kila siku.

Ameongeza kuwa, Yas inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya uhakika na yenye kasi zaidi popote pale walipo.

Kwa sasa kampuni inajivunia kuwa na mtandao mpana zaidi wa 4G nchini pamoja na upatikanaji wa teknolojia ya 5G katika miji ya kimkakati.

“Lengo letu ni kuhakikisha wateja wanaweza kuwasiliana bila kikwazo, kuendesha biashara zao kwa ufanisi na kupata taarifa kwa wakati, hasa katika mwezi huu mtukufu ambapo mawasiliano yana umuhimu mkubwa,” amesema.

Katika kuunga mkono ibada na mahitaji ya mwezi wa Ramadhani, Yas pia imetangaza kuwa huduma yake ya HIKMA, inayotoa elimu na maudhui ya dini ya Kiislamu, itapatikana bure kwa wateja wake katika kipindi chote cha mfungo wa Ramadhani.

Kupitia HIKMA, wateja wanaweza kusikiliza mafundisho kuhusu Laylatul Qadr, Zakatul Fitr, Eid-l-Fitr, faida za funga, dua mbalimbali, uradi na mafunzo ya swala ya Taraweeh.

Huduma hiyo  inapatikana kwa kupiga namba 0901655582 au kutuma SMS kwenda 15582.

Aidha, wateja watapokea SMS tano za ukumbusho wa nyakati za swala kila siku bila malipo.Kasulwa amesema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya kampuni kuendelea kuwa mshirika wa karibu wa jamii na kuunga mkono utamaduni na imani za Watanzania.

“Ramadhani ni muda wa kutafakari, kushirikiana na kujenga undugu. Kama kampuni, tunaheshimu sana thamani hizi, na ndiyo maana tumeweka kipaumbele kuwa karibu na jamii katika kipindi hiki,” ameongeza.

Amehitimisha kwa kuwaombea wananchi mfungo wenye amani, baraka na utulivu, akisisitiza kuwa kampuni itaendelea kushirikiana na wateja na jamii kwa ujumla katika shughulimbalimbali za kijamii.