Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma
CHAMA Cha Kulinda na Kutetea Haki za Walimu Tanzania(CHAKUHAWATA)Kimeiomba Serikali itoe maelekezo kwa waajiri kuwapa uhuru wafanyakazi kujiunga katika vyama vya wafanyakazi wavitakavyo.
Vilevile wameiomba serikali iingize Vyama vya Wafanyakazi kwenye mfumo wa ESS ili wafanyakazi waombe wenyewe kupitia mgumo huo ili kuondoa usumbufu unaoletwa na baadhi ya waajiri nchini pale mfanyakazi anapotaka kujiunga katika Chama cha wafanyakazi au kujiondoa.

Ambapo kimesema utaratibu huo utaondoa usumbufu na malalamiko kutoka kwa wafanayakazi.
Maombi hayo yametolewa jijini hapa leo Machi 14,2026 na Naibu Katibu Mkuu wa CHAKUHAWATA Abians Lutandika wakati akisoma taarifa fupi kwa mgeni rasmi katika Kikao cha Viongozi wa Chama hicho ambapo amesema maombi hayo ni kutokana changamoto zinazowakabili wanachama ambazo wanaamini zikifanyiwa kazi wananchama wao watafurahia zaidi.
Lutandika ametaja changamoto hizo kuwa ni baadhi ya Waajiri(Wakurugenzi) kutotoa ushirikiano kwa chama kwa kutoingiza makato ya Ada kwa wanachama ambao wamejiunga katika chama hicho baada ya kutimiza taratibu zote za kujiunga,licha ya kutambua kuwa mfanyakazi anayo haki ya kujiunga katika chama cha wafanyakazi au kuhama chama alichokuwa awali.

“Changamoto nyingine chama chetu kutoshirikishwa katika Mabaraza ya wafanyakazi yanayofanyuka katika Halmashauri.Baadhi ya waajiri kuwahamisha walimu ambao ni viongozi wa Chama chetu katika maeneo yao ya uongozi bila sababu za msingi na bila kuwapa stahiki zao za uhamisho,”amesema.
Aidha ametaja changamoto nyingine kuwa baadhi ya waajiri kuingiza makato ya vyama viwili vya wafanyakazi kwenye mishahara ya wanachama wao kinyume na nyaraka na sheria.
Pia ametaja Chama na wanachama kitoshirikishwa katika maadhimisho ya sherehe ya wafanyakazi duniani(Mei Mosi)na wakati mwingine kuwaondoa katika maandamano pale wanapokuwa wamejitokeza kushiriki katika maandamano na wafanyakazi wa vyama vingine ni jambo amabalo limekuwa likifanywa katika baadhi ya mikoa nchini.
“Naomba ieleweke kuwa vyama vya wafanyakazi vipo kwajili ya kutetea na kulinda maslahi mapana ya wafanyakazi hivyo hakuna haja ya waajiri nchini kuweka vikwazo vya kujiunga na vyama vya wafanyakazi kwani wanaba kwa kutumia uhuru wao wenyewe kwa mujibu wa sheria za nchi”Amesema Naibu Katibu mkuu wa Chama hicho.
Pamoja na hayo Naibu Katibu huyo amesema Chama hicho hadi kufikia mwezi Februari 2026 wameongeza idadi ya wanachama hadi kufikia 49,750 nchi nzima huku walimu zaidi ya 3000 wameomba kujiunga na chama hicho.
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu(ADEM) Dkt.Maulid Maulid ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi

katika kikao kazi hicho cha viongozi wa chama hicho kutoka Mikoa yote ya wanachama ameeleza kuwa chama hicho ni chama halali na kinatakiwa kufanya kazi zake kisheria ,kanuni na taratibu kwani kipo kwa ajili ya kusaidia walimu na serikali.
“Niwasihi CHAKUHAWATA kama chenu kipya umaarufu wenu utajijenga katika kudhibiti migogoro na waajiri na mtumie njia za majadiliano na kushauriana ili kuleta maelewano na mahusiano bora na waajiri na muweze kutimiza malengo yenu”amesema Dkt.Maulid.
Akizungumia changamoto ziliotajwa na chama hicho amesema kuwa ataziwasilisha kwa wakubwa wake wa kazi na ana uhakika kuwa zitafanyiwa kazi.
Naye Kamishna kutoka Tume ya Utumishi Walimu Mwantumu Mussa amwakumbusha Viongozi wa Chama hicho mambo yanayowaharibia mustakabali wao kuwa ni kutokujua wajibu wao kwani wanapaswa kujua watu wanaowasimamia.

“Ninyi mnawasimamia Walimu basi waelimisheni wajue sheria taratibu na kanuni ambao ndiyo msingi wao mkuu utakao waongoza katika utumishi wao,”amesema Mussa.

More Stories
Salome: Miradi ya umeme vitongoji yaanza kuzaa matunda Shinyanga
EWURA yatoa elimu uvunaji maji ya mvua kwa walemavu
Kamati ya Bunge yaridhishwa ujenzi kampasi ya Mzumbe