📌 Kiwanda chenye thamani ya Shilingi Bilioni 7.9 chaanza kuzalisha nguzo 80–120 kwa siku
Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeridhishwa na kukamilika kwa ujenzi wa Kiwanda cha Kutengeneza Nguzo za Zege cha TCPM kilichopo mkoani Tabora, ambacho sasa kimeanza rasmi uzalishaji wa nguzo hizo kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya usambazaji wa umeme nchini.
Katika ziara ya Kamati leo, tarehe 12 Machi 2026 ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Subira Mgalu , ilitembelea kiwanda hicho kinachomilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni yake tanzu ya TCPM.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo,Mgalu ameishauri Wizara ya Nishati kuweka mikakati ya kujenga viwanda zaidi vya nguzo za zege katika kanda mbalimbali nchini kwa kushirikiana na wawekezaji wa ndani ili kuongeza uzalishaji na kukidhi mahitaji ya taifa.

Ameeleza kuwa matumizi ya nguzo za zege katika usambazaji wa umeme yataongeza uimara wa miundombinu ya umeme na kupunguza changamoto ya kuoza au kuanguka kwa nguzo za miti, hali ambayo imekuwa ikisababisha hitilafu za mara kwa mara katika baadhi ya maeneo nchini.
“Tumeona mradi wa kihistoria ambao ni alama ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hii ni hatua kubwa na mapinduzi katika sekta ya nishati,” amesema Mgalu.

Awali, Waziri wa Nishati,Deogratius Ndejembi, ameeleza kuwa ujenzi wa kiwanda hicho ulianza Oktoba 2024 na kukamilika Februari 2026 kwa gharama ya shilingi bilioni 7.9.
Amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha nguzo za zege kati ya 80 hadi 120 kwa siku, hatua itakayosaidia kuongeza upatikanaji wa nguzo hizo nchini, hususan katika kipindi ambacho mahitaji ya TANESCO yanaendelea kuongezeka.
“Kwa sasa TANESCO imeanza kutumia kwa wingi nguzo za zege hasa katika maeneo ya mijini, maeneo oevu pamoja na maeneo yenye changamoto ya kuwaka moto wakati wa shughuli za kilimo,” amesema Ndejembi.

Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 TANESCO ilikuwa na uhitaji wa nguzo za zege 200,000, wakati uzalishaji wa sekta binafsi hauzidi nguzo 80,000, hali inayoonyesha bado kuna pengo kubwa la uzalishaji nchini.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Ndejembi amewakaribisha wawekezaji wa sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya nguzo za zege, akitaja ukanda wa Mbeya na maeneo mengine kuwa na fursa kubwa ya uwekezaji katika sekta hiyo.

More Stories
Kamati ya Kudumu ya Bunge Nishati ya Madini yaridhishwa na maendeleo ya kiwanda cha Nguzo za Zege
Wanawake vinara wapewa tuzo na Plan International kama sehemu ya kutambua michango yao
Mhandisi Saidy: Wananchi wanayomatumaini makubwa na REA