Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online, Mbarali
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya inaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, ambapo zaidi ya Shilingi bilioni 1.7 tayari zimenufaisha wanawake wilayani humo.
Mikopo hiyo inayotolewa na serikali inalenga kuwawezesha wananchi, hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujihusisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ili kuboresha maisha yao na kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli, amesema halmashauri hiyo imekuwa ikisimamia kwa karibu utekelezaji wa mikopo hiyo kwa kuzingatia maelekezo ya serikali pamoja na kanuni na taratibu za kisheria.

Amesema mpaka sasa wanawake pekee wamenufaika na mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 1.7, huku mikopo hiyo ikiendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali.
“Mwaka 2025 halmashauri ilitoa mikopo yenye thamani ya Shilingi milioni 500 na mwanzoni mwa mwaka huu tayari tumetoa Shilingi milioni 733. Bado kuna fedha zilizotengwa ambazo zitaendelea kutolewa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa,” amesema Mweli.
Ameeleza kuwa serikali imekuwa ikitambua kuwa si kila mwananchi anaweza kupata ajira rasmi, hivyo ina jukumu la kuweka mazingira yanayowawezesha wananchi kujihusisha na shughuli za kiuchumi zinazoweza kuongeza kipato chao pamoja na kuchangia pato la taifa.
Aidha, Mweli amesema hivi karibuni alitoa maelekezo kwa halmashauri kuandaa taarifa maalum itakayoonyesha kwa undani mafanikio na mabadiliko yaliyotokana na mikopo hiyo kwa wananchi wa wilaya ya Mbarali, hususan wanawake.
Kuhusu miundombinu, Mweli amesema halmashauri imeendelea kuboresha huduma za kijamii na kupunguza changamoto zilizokuwepo hapo awali.
Amefafanua kuwa kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025 hadi 2025/2026, halmashauri imepeleka zaidi ya Shilingi bilioni 2 katika miradi ya maendeleo ya sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari.
Pia amesema halmashauri imeanzisha utaratibu wa kufanya ziara za ukaguzi wa miradi ya maendeleo kila wiki katika kata mbalimbali ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ubora unaotakiwa.
Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Mbarali, Groly Komba, amesema katika kipindi cha mwaka mmoja halmashauri hiyo imetoa zaidi ya Shilingi bilioni 1 kwa vikundi 165 vya wanawake pekee.

Komba amesema halmashauri imekuwa ikiwahamasisha wanawake kuunda na kusajili vikundi rasmi pamoja na kupata vitambulisho ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali pamoja na taasisi za kifedha.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Bahati Ndingo, amesema Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ni fursa ya kutathmini hatua zilizofikiwa katika kuwawezesha wanawake kimaendeleo.
Amesema Tanzania kuongozwa na Rais mwanamke, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni ishara kubwa ya maendeleo katika kupigania haki na uwezo wa wanawake katika nafasi za uongozi.
“Kuongozwa na mwanamke shupavu kama Rais Samia kunaonyesha kuwa wanawake wana uwezo wa kuongoza katika ngazi za juu. Siku hii si ya kujitapa bali ni ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kushukuru mchango wa wanaume ambao wamebadili mtazamo wao kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii,” amesema Ndingo.

More Stories
Tafiti nne NBS kuboresha mazingira ya biashara,uwekezaji
Msichana Initiative yazindua mradi wa Renewed Women Voices and Leadership Tanzania
Msajili wa Hazina, Arise Investments kuimarisha uwekezaji NMB