March 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mvua yasababisha mafuriko Mwanza,watoto wanne waokolewa Mkuyuni

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

JIJI la Mwanza leo Machi 10,2026 limekumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia Machi 10,2026 yakiwa yamesababisha taharuki na kusimamisha shughuli nyingi za kiuchumi kwa saa kadhaa ikiwemo wananchi kukwamisha kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine.

Huku watoto wanne wa familia tofauti wakinusurika kifo baada ya kuokolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza,Kata ya Mkuyuni eneo lililoathirika zaidi na hata hivyo, mwili wa mwanamke mmoja ulipatikana ukiwa unaelea ndani ya Ziwa Victoria.

Kamanda wa Jeshi la Uokoaji na Zimamoto Mkoa wa Mwanza (RFO),Elisa Mugisha,Machi 10,2026, katika mahojiano na Majira,amesema kwamba mafuriko hayo yalisababishwa na mvua kubwa zilizoanza kunyesha majira ya saa 9:30 usiku.

Amesema kuwa, mvua hizo zilisababisha barabara za Mkuyuni na Butimba kufungwa ili kuepusha madhara kwa watumiaji wa vyombo vya moto na maisha ya wananchi wakiwemo wakazi wa Kata za Butimba na Mkuyuni.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo wa Zimamoto na Uokoaji, baadhi ya magari ambayo madereva wake walilazimisha kupita ndani ya maji ya mafuriko yaliyokuwa yakipita juu ya daraja la Mkuyuni, zilikuwa zikielea na kulazimika kuvutwa baada ya kuzima.

“Maeneo yaliyoathirika ni Nyamh’ongolo, Mkuyuni na Butimba. Watu walilazimika kupanda juu ya kuta na mapaa ya nyumba zao kujiokoa, huku watoto wanne wakiondolewa kutoka ndani ya nyumba zilizozungukwa na maji,”amesema Mugisha.

Amesema miongoni mwa watoto waliokolewa, mmoja wa jinsia ya kike mwenye umri wa miezi minne alipelekwa,hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza,Sekou-Toure,huku wengine watatu waliokuwa pekee yao bila wazazi wao, wakipatiwa msaada na askari wa kikosi hicho cha uokoaji.

Kamanda Mugisha ameeleza kuwa, licha ya madhara makubwa ya mali, hakuna kifo kilichotokea miongoni mwa binadamu isipokuwa mwili wa mwanamke aliyepatikana Ziwa Victoria, huku akisisitiza kuwa wataendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na hasara ya mali na madhara mengine kutokana na mafuriko hayo.

Mugisha ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari na kuhakikisha ujenzi wa makazi yao unazingatia michoro, pamoja na kutumia namba za dharura kupata msaada wa haraka.

 “Tumepokea simu nyingi za kuomba msaada, tofauti na zamani ambapo wengi hawakujua nini cha kufanya,hivyo ,naamini elimu yetu imewafikia wananchi na wakazi wengi,”amesema.

Aidha, baadhi ya wananchi wamesema kuwa mvua hiyo iliathiri familia nyingi za Mkuyuni na Butimba, hasa zile zinazoishi kando ya mto unaotiririsha maji kwenye daraja la Mkuyuni ambalo lilifanyiwa marekebisho na kujengwa na JASCO.

“Tatizo kubwa ni miundombinu isiyo rafiki ya daraja lililojengwa Mkuyuni, ambalo halipitishi maji vizuri,”amesema Asha Shaaban, mmoja wa waathirika.

 Chacha Getonga,amesema mvua hiyo ambayo imeanza kunyesha kuanzia majira ya alfajili mpaka saa saba mchana,imewapa usumbufu watumiaji wa barabara hiyo hususani katika daraja hilo la Mkuyuni.

Amesema, kufuatia hali hiyo wameshindwa kuvuka kwenda upande mwingine hivyo baadhi wamelazimika kurejea nyumbani na hivyo siku yao imeisha bila kuingiza kipato.

Bertha Rock,amesema alikuwa anaelekea stendi ya mabasi Nyegezi ili kupanda basi kuelekea Katoro mkoani Geita,ila baada ya daladala aliyokuwa amepanda kufika stendi ya Igombe mjini kati,Askari wa Usalama Barabarani aliwasimamisha na kuwazuia wasiendelee na safari kwani daraja alipitiki maji yamejaa.

“Nimelazimika kurudi Kamanga kuona namna ya kuvuka na kivuko hadi Sengerema,lakini nilivyofika hapo kwa bahati nikakuta basi linaloenda Geita ambalo limesema linapitia njia Igoma -Kishiri mpaka Buhongwa kisha tunaendelea na safari,ingawa inakuwa ni kuzunguka sana,”amesema Bertha.

Naye mwanaume mmoja alijitaja kwa jina la Baba Nelly,amesema ipo haja ya Serikali kuangalia upya namna ya kushughuliki changamoto ya maji kujaa katika daraja hilo la Mkuyuni,ambapo amedai kuwa walitegemea baada ya uboreshaji hali hiyo isinge tokea.

“Japo mimi siyo mtaalamu Serikali ingeona namna ya kushughulikia changamoto katika daraja hili ambalo linaonekana kama mlango wa kuingilia ziwani nauwenda mto wake unapokea maji mengi zaidi,”amesema Baba Nelly.