March 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARURA yaboresha miundombinu Karatu

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online -Karatu

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Karatu,umeendelea kuboresha miundombinu  kwa kujenga barabara za lami ndani ya mji huo, hatua inayolenga kurahisisha usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Huku waendesha bodaboda wakitakiwa kupunguza mwendo kufuatia kuimarika kwa barabara hizo ili kuepuka ajali zinazoweza kusababisha vifo au majeraha.

Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA Wilaya ya Karatu ,Mhandisi Msetu Madara,wakati akiongea na waandishi wa habari wilayani hapo,ambapo alisema,TARURA wilayani humo inahudumia jumla ya Kilomita 771 za barabara.

Kati ya Kilomita hizo  barabara za lami ni Kilomita 4.34 zilizopo katika mji  mdogo wa Karatu, barabara za changarawe Km. 315.816 na udongo ni Km. 451.400.

“Tunajitahidi kuhakikisha barabara za Karatu zinakuwa nzuri na zinapitika majira yote ya mwaka.Kwani ni mji wa kitalii unaopokea watalii wengi wanaotembelea vivutio vya utalii kama Hifadhi ya Ngorongoro na Serengeti.Mkakati wetu ni kuhakikisha mji wote unakuwa na barabara za lami,”amesema Mhandisi Madara.

Mhandisi Madara,amesema wakala huo unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara mpya za lami ndani ya mji huo,barabara za lami zenye urefu wa kilometa 1.4 ambazo zimejengwa hivi karibuni zimejengwa mitaro ya maji katika pande zote mbili za barabara hizo ili kulinda miundombinu dhidi ya uharibifu.

 Pia kuna mpango wa kuweka taa za barabarani katika barabara mpya ili kuimarisha usalama wa watumiaji wakati wa usiku na kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika hadi nyakati za usiku.

Aidha,amesema hivi sasa wamekamilisha ujenzi wa daraja la mawe la Chemchem lililopo kiijiji cha Chemchem lenye urefu wa mita 21 na upana wa mita 7,ujenzi huo unaambatana na barabara yenye urefu wa Km tano, inayounganisha vijiji vya Endallah, Manusai, Masabeda, Endamarariek, Basodawishi, Chemchem, Kilimamoja, Gidibaso, Getamock, Qaru na Endabash.

Ameongeza kuwa hadi Februari mwaka huu, TARURA imefanikiwa kujenga madaraja sita ili kuondoa vikwazo vya usafiri na kurahisisha wananchi kupata huduma za kijamii.

Hata hivyo, TARURA inaendelea kutoa elimu kwa wananchi, hususan vijana wanaoendesha pikipiki, kuendesha kwa mwendo unaozingatia usalama barabarani ili kuepuka ajali. Alisisitiza kuwa vijana hao wanapaswa kutambua kuwa wao ni nguvu kazi ya Taifa na wanapaswa kujilinda.

Kwa upande wake,Msimamizi wa miradi hiyo, Mhandisi Daines Simba,amesema  awali mji wa Karatu haukuwa na barabara za lami lakini sasa wamefanikiwa kujenga miundombinu hiyo ambayo imechochea ukuaji wa uchumi wa wananchi na kuajiri vijana katika kazi za ujenzi.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mjini Kati, Elisifa Amma,amesema awali  eneo hilo lilikuwa na barabara mbovu zilizokuwa na mashimo na matope hali iliyokuwa ikisababisha usumbufu kwa wananchi.

“Magari mengi sasa yanapita kwa urahisi yakileta watalii, hali ambayo imeongeza biashara. Hata fremu za maduka sasa zinapangishwa kwa urahisi kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi,” amesema.

Kwa upande wake,Salome Minja ambaye ni mjasiriamali wa mgahawa katika Mji wa Karatu,amesema awali ubovu wa barabara uliwakosesha wateja kutokana na matope wakati wa mvua na vumbi wakati wa kiangazi lakini sasa hali imebadilika mji umechangamka na biashara zinaendelea vizuri.