September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Afisa Mtendaji wa Bodi ya Ligi Tanzania Bara, Almas Kasongo

Wanaotumia viwanja vibovu wajiandae

AFISA Mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB), Almas Kasongo amesema wataendelea kufungia viwanja vyote vitakavyoonekana kutokidhi viwango vya kutumika kwa ajili ya mechi za mashindano mbalimbali.

Kasongo ametoa kauli hiyo baada ya juzi Bodi hiyo kutangaza kuufungia uwanja wa Jamhuri, Morogoro hadi pale utakapofanyiwa marekebisho mara baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya wenyeji Mtibwa Sugar na Yanga ambao walipata ushindi wa goli 1-0.

Sababu kubwa za kufungiwa kwa uwanja huo ni eneo la kuchezea (pitch) kutokuwa zuri, kuwepo kwa kasoro katika vyumba vya kubadilishia nguo pamoja na sehemu za kukaa wachezaji wa akiba na maafisa wa benchi la ufundi wakati ya mchezo kutokuwa na ubora.

Uwanja huo unakuwa wa tano kufungiwa baada ya kutangaza kufungia uwanja wa Gwambina, Kumbukumbu ya Karume mkoani Mara, uwanja wa Mabatini pamoja na ule wa Chuo cha Ushirika uliopo Moshi.

Akizungumza na Mtandao huu, Kasongo amesema, wapo radhi kubaki na viwanja vichache vyenye ubora kwani wao kama viongoozi watahakikisha wanafungia viwanja vyote ambavyo havina ubora kikanuni kuwa katika sheria namba moja kwani wamebaini vingi vina mapungufu.

“Kama tulifanya makosa nyuma hatuwezi kukubali kuyarudi na ndio maana tumechukua haya maamuzi magumu kwani ni lazima tufike sehemu mpira uchezwe katika mazingira ambayo kila mtu atatani acheze, ” amesema Kasongo.

Hoja ya kuwa kwanini uwanja ufungiwe sasa haina mashiko kwani walishaona mapungufu yanayokiuka sheria namba moja ya uwanja na ndio maana wanaomba kuungwa mkono katika hilo.

Amesema, akiwa kama Mtendaji mkuu atahakikisha anaendelea kusimamia jambo hilo kwani pamoja na yote yanayozungumzwa hivi sasa na bado yatakuwepo mengine lakini ni lazima wasimame kwenye hoja ya msingi ya kusimamia sheria.

“Kazi yangu ni kusimamia Ligi ili kuona inachezwa katika viwanja vinavyokidhi matakwa tuliyojiwekea na kinachowafariji ni kuona tunajiridhisha kiwanja tulichokifungia kweli hakistahili hivyo ni lazima tufike pale tunapopatarajia, ” amesema Kasongo.