Mwandishi: Ismail Mayumba
Kadri dunia inavyoendelea kukua na kupiga hatua katika nyanja ya teknolojia, ndivyo binadamu pia analazimika kuendana na mabadiliko hayo. Katika kipindi cha sasa, karibu huduma zote muhimu iwe ni za kiserikali au zisizo za kiserikali zinapatikana kupitia mifumo ya kidijitali na mifumo ya mtandaoni. Huduma kama za kifedha, afya, elimu, ajira, usajili wa taarifa binafsi na hata huduma za kiusalama hutegemea sana matumizi ya teknolojia.
Ili kuweza kufikia huduma hizo, umiliki wa simu janja umekuwa ni jambo la lazima kwa watu wengi. Hata hivyo, simu haiwezi kufanya kazi bila kuwepo kwa laini ya mawasiliano. Hapo ndipo zoezi la kusajili laini za simu linapopata umuhimu wake mkubwa katika maisha ya kila siku ya mwananchi.
Zoezi la kusajili laini ya simu kwa mtazamo wa juu linaonekana kuwa ni rahisi na la muda mfupi. Hata hivyo, kwa undani zaidi, zoezi hili linabeba uzito mkubwa sana kwa sababu linahusisha utambulisho wa mtu mmoja mmoja mtandaoni. Laini ya simu inapotumika vibaya, madhara yake humrudia yule ambaye taarifa zake zilitumika kuisajili laini hiyo.
Kwa bahati mbaya, wapo baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu wanaotumia nafasi ya kutokujua au uzembe wa wananchi kujipatia kipato kwa njia zisizo halali. Kitendo cha kujitafutia riziki si tatizo, ila tatizo hujitokeza pale mtu anapojinufaisha kwa njia ambayo inamuweka mwananchi mwingine katika matatizo makubwa ya kisheria na kiusalama.
Utaratibu wa usajili wa laini za simu nchini hutumia Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIDA). NIDA inapowasilishwa wakati wa usajili, mfumo huvuta taarifa zote muhimu za mhusika ikiwemo jina, picha, alama za vidole na taarifa nyingine binafsi. Endapo itatokea mtu mwingine akasajili laini kwa kutumia NIDA yako bila idhini yako, basi wewe ndiye unayetambulika kisheria kama mmiliki wa laini hiyo. Matokeo yake, vitendo vyote vitakavyofanywa kwa kutumia laini hiyo ikiwemo uhalifu wa mtandaoni vitahusishwa moja kwa moja na wewe.
Hali hii huwapa nafasi wahalifu kufanya uhalifu mtandaoni kwa kujiamini, wakijua kuwa hawatatambulika moja kwa moja kwa sababu wanatumia utambulisho wa mtu mwingine. Hii imekuwa chanzo kikubwa cha matatizo kwa wananchi wengi wasio na hatia.
Mojawapo ya mbinu zinazotumiwa na watu wasio waaminifu wakati wa kusajili laini ni udanganyifu. Mwananchi anapofika kusajili laini, huombwa kuweka alama ya kidole. Baada ya kufanya hivyo mara ya kwanza, huambiwa kuwa “mtandao umesumbua” na kuombwa ajaribu tena. Anapojaribu mara ya pili, usajili unaonekana kufanikiwa. Hata hivyo, ukweli ni kwamba usajili wa kwanza ulikubaliwa, lakini laini hiyo hufichwa pembeni bila mhusika kujua, kisha anapewa laini ya pili. Baadaye, yule msajili huja kuiuza ile laini ya kwanza kwa mtu mwingine kwa bei kubwa.
Mnunuzi wa laini hiyo anaweza kuitumia kufanya uhalifu wa aina mbalimbali, ikiwemo utapeli, uhalifu wa kifedha au uhalifu mwingine wa mtandaoni. Mwishowe, faida huenda kwa yule msajili mdanganyifu, lakini madhara yote humrudia mwananchi ambaye NIDA yake ilitumika. Inaweza kufikia hatua mtu akiwa nyumbani kwake, ghafla vyombo vya dola vinamkamata kwa tuhuma za uhalifu ambao hajawahi kuufanya.
Kwa sababu hiyo, ni muhimu sana kwa kila mwananchi kuchukua tahadhari. Njia rahisi ya kujua namba za simu zilizosajiliwa kwa kutumia NIDA yako ni kwa kupiga *106#. Huduma hii hukuwezesha kuona orodha ya laini zote zilizosajiliwa chini ya utambulisho wako. Endapo utaona namba usiyoitambua, ni vyema kuchukua hatua haraka kwa kutoa taarifa kwa polisi au kwa kampuni husika ya mawasiliano ya simu ili hatua stahiki zichukuliwe.
Kwa sasa, kumekuwepo na maboresho makubwa ya kiteknolojia ikilinganishwa na hapo awali. Mfumo unatambua pia ni msajili gani amesajili laini husika. Endapo itabainika kuwa msajili alitoa laini kwa mtu mwingine kinyume cha sheria na uhalifu ukafanyika, basi wote wawili msajili na mtumiaji wa laini wanaweza kukamatwa na kuhojiwa kwa mujibu wa sheria.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pia imechukua hatua madhubuti kudhibiti tatizo hili kupitia oparesheni mbalimbali, ikiwemo Oparesheni Tokomeza. Katika oparesheni hiyo, maafisa wa TCRA walijifanya kama raia wa kawaida waliotaka kusajili laini. Wale wote waliobainika kusajili laini kwa njia za magendo walichukuliwa hatua za kisheria. Hatua hii ilisaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza vitendo hivyo hadi kufikia hali ya sasa.
Kwa usalama wako binafsi, inashauriwa mwananchi asajili laini zake katika vituo rasmi vya kampuni za simu. Endapo italazimika kusajili kwa wakala wa mtaani, hakikisha unamsajili anayefahamika na unayemuamini. Baada ya kukamilisha usajili, ni muhimu kupiga *106# mara moja ili kuthibitisha namba zilizosajiliwa kwa NIDA yako.
Kwa kufanya hivyo, utakuwa umejilinda dhidi ya madhara ya uhalifu wa mtandaoni na kutumia teknolojia kwa usalama na ufanisi zaidi.

More Stories
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi