Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Kahama
Waendesha bodaboda, bajaji za abiria na mizigo (GUTA) pamoja na Umoja wa Mafundi Ujenzi Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, wameahidi kushiriki katika ujenzi wa ofisi za serikali za mitaa zilizoharibiwa kwa moto wakati wa vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025 katika uchaguzi mkuu.
Ahadi hiyo walitoa Machi 4,2026,mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Freck Nkinda, baada ya ziara ya kuwatembeza katika majengo ya ofisi za kata zilizoteketezwa kwa moto Oktoba 29 ,2025 katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama.

Ambapo walitembelea Kata za Malunga, Mhungolo, Majengo, Nyasubi, Mhungula na Shunu, ambazo zote ziliripotiwa kuharibiwa vibaya kwa moto.
Akizungumza na vijana hao, Nkinda,amesema uharibifu wa mali hizo za umma umeleta kero na adha kwa wananchi kupata huduma za msingi, pia ukiwaathiri wasafirishaji hao wanaotegemea ofisi hizo kwa huduma mbalimbali za kijamii na kiutawala.
Amesema aliamua kuwaita na kuwashirikisha ili wajionee wenyewe uharibifu uliofanyika katika kata hizo,na amesisitiza kuwa Serikali ilijenga ofisi hizo kwa nguvu na kodi za wananchi, hivyo si sahihi kuanza mchakato wa ujenzi bila wao kushuhudia hasara iliyotokea.
“Serikali ilitumia fedha za walipa kodi kujenga miundombinu hii. Ni muhimu kila mmoja atambue thamani yake na kushiriki katika kuirejesha,”amesema Nkinda.
Diwani wa Kata ya Kahama Mjini, Gardison Andrew,amewataka vijana kuwa chachu ya maendeleo kwa kuzingatia upendo, amani, umoja na mshikamano, huku wakiacha vitendo vya vurugu vinavyorudisha nyuma juhudi za maendeleo ya Serikali na jamii .

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Waendesha Bodaboda Mkoa wa Shinyanga, Iddsam Mapande,amesema wapo tayari kutoa mchango wao wa nguvu kazi na rasilimali walizonazo ili kuhakikisha ofisi hizo zinajengwa upya haraka iwezekanavyo.
Naye Kiongozi wa Waendesha Bajaji, Richard Malifedha,amesema wanaunga mkono jitihada za Serikali na wapo tayari kushiriki katika ujenzi huo pale watakapohitajika.
Nao baadhi ya wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama,wamesema kuharibiwa kwa ofisi za kata kumewasababishia adha na usumbufu pindi wanapohitaji huduma za msingi katika maeneo yao, huku wakilaani vitendo vya uharibifu vilivyosababisha hasara hiyo.

More Stories
Silinde azindua baraza la sita la Wafanyakazi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini