March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilemela yavuka lengo uandikishaji darasa la kwanza

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza,imefanikiwa kuandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza 14,134,sawa na asilimia 102 ya maoteo kwa muhula wa masomo wa mwaka 2026.

Hivyo wamevuka lengo la uandikishaji ambapo kwa mujibu wa maoteo ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), halmshauri hiyo ilipaswa kundikisha wanafunzi wa darasa la kwanza 14,087,kwa mwaka wa masomo 2026.

Akizungumza na Majira Machi 3,2026,Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu,Divisheni ya Awali na Msingi Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Hellen John,amesema zoezi la uandikishaji wanafunzi wa awali na msingi kwa mwaka wa masomo 2026, lilianza Oktoba 2025 na linatarajiwa kukamilika Machi 31,mwaka huu.

Hellen,amesema kwa mwaka 2026 kwa maoteo ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ilipangiwa kuandikisha wanafunzi wa awali 14,393 huku wa darasa la kwanza 14,087.

Amesema mpaka Februari 26,2026 wameisha andikisha wanafunzi wa awali 12,420 kati yao wavulana 6,249 na wasichana 6,171,sawa na asilimia 86.

Huku kwa darasa la kwanza wameisha andikisha wanafunzi 14,134,kati yao wavulana 6,911 na wasichana 7,223 sawa na asilimia 102, hivyo wamevuka lengo la maoteo ambayo walipaswa kuandikishwa wanafunzi 14,087.

“Miongoni mwa wanafunzi hao wapo wenye mahitaji maalumu kwa maana ya ulemavu tofauti,ambapo kwa awali tumeandikisha wanafunzi 26 na wanafunzi 59 kwa darasa la kwanza,”amesema Hellen.

Sanjari na hayo Hellen,amesema,Kata ya Pasiansi imefanya vizuri katika zoezi la uandikishaji ambapo ilipangiwa kuandikisha wanafunzi 375 mpaka Februari 26,2026 walikuwa wameandikisha wananfunzi 494 sawa na asilimia 132, Kata ya Bugogwa imeandikisha kwa asilimia 129,Nyasaka asilimia 117, Buzuruga asilimia 125, Nyamanoro asilimia 118.

Huku Kata ya Kirumba ikiwa chini imeandikisha kwa asilimia 51,ambapo ilipaswa kuandikisha wanafunzi 405 na mpaka sasa wameisha andikisha wananfunzi 208.

Mwalimu Mkuu shule ya msingi Bulola, Fredrick Kakinda,amesema muitikio wa wazazi kuandikisha wanafunzi wa awali na msingi upo vizuri na inachangiwa na matokea mazuri ya madarasa ya mtihani hususani la saba na la nne.

Mwalimu Kakinda,amesema mwaka jana walikuwa na idadi ya wanafunzi wachache lakini mwaka huu ni wengi,ambapo kwa darasa la awali mwaka jana wanafunzi 78 na darasa la kwanza 135.

Mwaka huu wanafunzi wa darasa la awali mpaka sasa wameisha andikisha 88, wasichana 43 na wavulana 45,maoteo ya kuandikishwa ni 70,hivyo wamevuka lengo sawa na asilimia 125.

“Darasa la kwanza walioandikishwa ni 145, maoteo ni wanafunzi 120, hivyo tumevuka lengo kwa asilimia 120, na mwaka jana wa walioandikishwa kwa darasa la kwanza ni 135.Mpaka mwishoni mwa Machi idadi itaongezeka,”amesema Mwalimu Kakinda.