September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uwanja wa Mkwakwani kujengwa upya

Na Steven William, Muheza

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia amesema kuwa wanamkakati mkubwa wa kujenga upya Uwanja wa Mkwakwani uliopo jijini Tanga ili kuwa cha kisasa zaidi na kimataifa.

Akizungumza na Mtandao wa Times Majira, Karia amesema, tayari ameshazungumza na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella na wadau wa soka Tanga kuangalia uwezekano wa kujenga upya uwanja huo.

Amesema, mpango uliopo sasa ni kuzungumza na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa ambao ndio wamiliki wa uwanja huo ili watoe ridhaa ya kukarabatiwana kuwa kama uwanja wa Mkapa.

Katika ukarabati wa uwanja huo, watatumia fedha za wadau mbalimbali ambao watajitokeza kusaidia juhudi hizo kwa kushirikiana na TFF ili kuhakikisha wanapandisha soka katika mkoa wa Tanga kama ilivyokuwa miaka iliyopita kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo kati ya Coastal Union na African Sports ambazo zote zinatumia uwanja huo.

“Lengo la TFF ni kuhakikisha inakarabati viwanja vyote vya kuchezea mpira katika nchi hii hata kule katika Wilaya pindi fedha tutakapopatikana lakini pia nawaomba wadau wa michezo wenye uwezo kujitokeza kuchangia kukarabati viwanja vya mpira ili kuwa vya kisasa na serikali itaweka mchango wake,” amesema Karia.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Muheza, Mohamed Moyo amemshukuru Karia kwa maandalizi yake ya kujenga upya uwanja wa Mkwakwani kuwa wa kisasa kwani sasa wataona mechi za kimataifa.

Amesema, pia wanamuomba kuangalia uwanja wa mpira ya Jitegemee uliopo Wilayani Muheza ambao umechakaa kabisa kwani sehemu ya kuchezea (Pitch) haina nyasi na kuta zake zimebomoka.

Mkurugenzi wa Hotel ya Tanga Beach Resort Hamisi Kindoroko amesema, kitendo cha TFF kukarabati upya uwanja wa Mkwakwani, kutawapa faraja kwani wanaamini utakapokamilika watapata fursa na kuona mechi za kimataifa katika uwanja huo.

Kwa upande wake, Charles Mhilu ambae ni mdau wa soko Wilayani Muheza amesema, Karia amefanya jambo muhimu sana kupigania kujenga upya uwanja wa Mkwakwani kwani utakuwa wa kisasa.

Amesema, pia wanamuomba rais huyo kufika katika Wilaya ya Muheza kutembelea na kukagua uwanja wa Jitegemee ambao una hali mbaya na kuta zake zimebomoka na katikati umekuwa kipara kabisa.

Tayari mgombea ubunge katika Jimbo la Muheza, Hamisi Mwinjuma ‘Mwana FA’ ameahidi kuufanyia ukarabati mkubwa uwanja huo wa Jitegemee endapo atapana nafasi ya Ubunge ili kukuza zaidi shughuli za michezo.