Na Joyce Kasiki,Timesmajira online Dodoma
NAIBU wa Wizara ya Fedha, Laurent Luswetula, ameielekeza Bodi ya Usimamizi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kutumia teknolojia zilizopo kuongeza ufanisi katika uzalishaji na usambazaji wa takwimu rasmi ili kuziba pengo la takwimu katika sekta mbalimbali.
Luswetula ametoa maelekezo hayo Leo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Bodi ya tatu ya NBS .
Amesema bodi ina utaalamu na uzoefu wa kutosha huku akiwataka wajumbe wake kushirikiana kikamilifu kuimarisha tasnia ya takwimu pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa takwimu bora kwa ajili ya mipango ya kisekta na kitaifa.
Awali ,Mtakwimu Mkuu, Dkt Amina Msengwa amesema, ofisi inaandaa Mpango Mkakati wa Tatu kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya takwimu.
Ameeleza kuwa, tasnia ya takwimu inaendelea kukua sambamba na maeneo mapya ya tafiti na ukusanyaji wa takwimu, na kwamba mpango huo utawezesha uzalishaji wa takwimu za kupima utekelezaji wa maono ya Dira ya Taifa ya 2050 na mipango mingine ya maendeleo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa takwimu za wakati halisi kwa ajili ya maamuzi sahihi, akibainisha kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeendelea kuimarisha mifumo ya kiteknolojia ili kukusanya na kusambaza takwimu kwa wakati.
Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Anne Makinda amesema, bodi itasimamia uwajibikaji ili kuhakikisha uzalishaji wa takwimu bora zinazokidhi viwango vya Kitaifa na Kimataifa kwa ajili ya maamuzi yanayotegemea ushahidi.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama