March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia aomboleza kifo cha Kardinali Pengo

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-es-Salaam  kilichotokea usiku wa Februari 19, 2026, katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar.

Taarifa iliotolewa Februari 20,2026 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu,Bakari  Machumu,imesema 

Rais Dkt. Samia anamkumbuka Kardinali Pengo kama kiongozi wa kiroho na mzalendo aliyetoa mchango mkubwa katika kuimarisha imani.

Pia maadili, umoja na mshikamano wa kitaifa, kupitia uongozi wake wa muda mrefu ndani ya Kanisa Katoliki.

Dkt.Samia,amesema taifa limepoteza kiongozi aliyelitumikia kwa uadilifu na kujitolea,mchango wake katika malezi ya kiroho na maadili utaendelea kukumbukwa, kuthaminiwa na kuenziwa.

Hivyo kupitia kifo hicho,Dkt. Samia ametuma salamu za rambirambi kwa Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, OFMCap Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam; Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), viongozi wa dini, pamoja na waumini wote walioguswa na msiba huu mzito.

Aidha,anaungana na Kanisa, waumini na Watanzania wote kwa ujumla katika kipindi hiki cha majonzi, na anamuomba Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya Marehemu mahali pema peponi, Amina.