March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanawake wa milimani waendelea kuumia licha ya ahadi za COP29

Na Martha Fatael, TimesMajira Online

Safari ya kila siku ya kutafuta maji na chakula

“Tunategemea mlima kwa chakula, maji na kuni, lakini hakuna anayetuambia ahadi za serikali zinatusaidiaje,” anasema Rehema Mollel (46), mkulima na mama wa watoto wanne, mkazi wa Kijiji cha Kalimani, Wilaya ya Siha, mteremko wa Mlima Kilimanjaro.

Kijiji cha Kalimani,kinasumbuliwa na ukame wa mara kwa mara, chemchemi nyingi zimekauka, na misitu imepungua, hali inayowalazimisha wanawake kama Rehema kutembea umbali mrefu kutafuta maji safi na kuni.

“Kauli yake inaakisi hali ya wanawake wengi wa milimani nchini, miaka miwili baada ya Tanzania kushiriki COP29 na kutoa ahadi za kuzingatia usawa wa kijinsia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ahadi za COP29: Sauti lakini hapana matokeo

Miaka miwili baada ya Tanzania kushiriki kwenye mkutano wa COP29 na kutoa ahadi za kuzingatia usawa wa kijinsia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hali halisi bado haijaonesha mabadiliko.

Wanawake wa milimani wanaendelea kuwa mstari wa mbele bila msaada mahususi wa kifedha, teknolojia au mifumo ya ulinzi wa kijamii inayotambua mchango wao.

Katika COP29, Tanzania ilijiunga na mataifa mengine kuunga mkono ajenda ya Gender-Responsive Climate Action, ikiahidi kuhakikisha wanawake wanashirikishwa kikamilifu katika upangaji na utekelezaji wa sera za tabianchi, hususani katika maeneo yaliyo hatarini kama milimani.

Ahadi hizo zililenga kutambua mzigo mkubwa unaowakabili wanawake katika kukabiliana na ukame, mmomonyoko wa ardhi na kupungua kwa uzalishaji wa chakula.

Hata hivyo, hali halisi katika maeneo ya milimani bado inaonesha pengo kubwa kati ya sera na utekelezaji. Wanawake wanaendelea kuwa mstari wa mbele kukabiliana na athari za tabianchi bila msaada mahususi pwa kifedha, teknolojia wala mifumo ya ulinzi wa kijamii inayotambua mchango wao.

Msaada wa wataalamu na uwajibikaji ni muhimu

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa mazingira uliofuatia COP30, Mjumbe wa Kikosi cha Majadiliano cha Afrika kuhusu Tabianchi (AGN), Dkt. Richard Mayungi,anasisitiza kuwa masuala ya jinsia hayawezi kutenganishwa na ulinzi wa mifumo ya ikolojia ya milimani.

Anaeleza kuwa bila kuweka wanawake katikati ya suluhu za tabianchi, ahadi za kimataifa zitabaki kuwa nadharia zisizoleta mabadiliko katika maisha ya wananchi.

“Masuala ya jinsia hayawezi kutenganishwa na ulinzi wa mifumo ikolojia ya milimani. Bila kuweka wanawake katikati ya suluhu za tabianchi, ahadi za kimataifa zitabaki kuwa nadharia zisizoleta mabadiliko katika maisha ya wananchi.”anasema

Kauli hiyo inaungwa mkono na mratibu wa shirika la kiraia linalofanya kazi na wanawake wa milimani Kaskazini mwa Tanzania, Bi. Leah Mushi, anayesema wanawake bado hawajapewa nafasi katika kamati za maamuzi kuhusu matumizi ya ardhi, misitu na rasilimali za maji. Kwa mujibu wake, miradi mingi ya tabianchi bado inaongozwa na wanaume, huku wanawake wakibaki kuwa walengwa bila sauti.

Changamoto halisi na kutokuwepo kwa uwajibikaji

Hadi sasa, wanawake wa milimani wanasema hawajaona mabadiliko yanayogusa maisha yao ya kila siku. Hakuna mifuko mahsusi inayowafikia moja kwa moja wala programu zinazoimarisha uwezo wao wa kiuchumi ili kukabiliana na athari za tabianchi.

Kwa wachambuzi wa masuala ya mazingira, tatizo kubwa si ukosefu wa sera bali ni uwajibikaji katika utekelezaji. Bila mifumo ya wazi ya kufuatilia ahadi za COP29 kuhusu jinsia, wanawake wa milimani wataendelea kubeba mzigo wa tabianchi huku sauti zao zikibaki nje ya majadiliano ya kitaifa.

Katika jitihada za kupata maelezo kutoka ngazi ya utekelezaji wa ndani, mwandishi aliwasiliana na afisa habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Zakayo Mosha ili kufahamu hatua zilizochukuliwa kutekeleza ahadi za COP29 zinazolenga wanawake wa milimani na changamoto ya upatikanaji maji. Hata hivyo, hadi makala hii inapochapishwa, halmashauri hiyo haikuwa imetoa majibu yoyote rasmi kuhusu changamoto hizo licha ya kutafutwa mara kadhaa.

Ahadi zinapopaswa kuonekana katika maisha halisi

Kwa Rehema, Elikanani Sumari na wanawake wengine wa milimani, wanasema ahadi za kimataifa zina maana pale tu zinapobadilika kuwa maji karibu na makazi yao, ardhi salama ya kilimo, na nafasi ya kushiriki maamuzi yanayoathiri maisha yao. Hadi hapo, COP29 itaendelea kubaki kumbukumbu ya kauli nzuri, lakini si mabadiliko halisi kwenye ardhi ya milima ya Tanzania.