Mwandishi: Ismail Mayumba
Katika ulimwengu wa kidijitali wa sasa, watu wengi wameanza kutumia majukwaa ya mtandaoni kufanya biashara mbalimbali. Mojawapo ya majukwaa yanayotumika kwa kiasi kikubwa ni Telegram. Biashara nyingi zimehamia kwenye jukwaa hili, hasa zile zinazohitaji kiwango kikubwa cha usiri, ambapo wahusika hawataki kujulikana wala taarifa zao kufahamika. Baadhi ya biashara hizi huhusisha miamala ya kifedha au utoaji wa fedha bila kuhusisha mifumo ya kiserikali, hususan kwa lengo la kukwepa kodi. Hivi karibuni, biashara za usambazaji wa video zisizo na maadili zimeonekana kuenea zaidi kupitia jukwaa la Telegram.
Miongoni mwa shughuli maarufu sana zinazofanyika Telegram ni mchezo wa upatu. Watu wengi wamevutiwa kujiunga na mchezo huu na pia kushawishi wengine wafanye hivyo. Upatu ni mfumo wa jadi wa kuchangiana fedha kati ya kundi la watu kwa makubaliano maalum. Hata hivyo, upatu unaoendeshwa kupitia Telegram unatofautiana na upatu wa asili. Katika mfumo huu, mtu hulipwa fedha pale anapowaleta watu wengine kujiunga, na endapo wale aliowaleta watawaleta wengine zaidi, kiasi cha fedha huongezeka maradufu. Aidha, michango hukusanywa kwa vipindi maalum kama vile kila siku, kila wiki au kila mwezi.
Kwa mtazamo wa haraka, mchezo huu huonekana kuwa rahisi na wenye faida kubwa, lakini kwa hakika ni kama mtego wa panya; mwanzoni mtu hunufaika, lakini kadri mfumo unavyoendelea, hushawishiwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha. Hatimaye, waendeshaji wa mchezo hupotea bila kujulikana, na waathirika hubaki wakihangaika kutafuta haki yao.
Mbali na mchezo wa upatu, Telegram pia hutumika kama jukwaa la biashara ya ngono, ambapo baadhi ya wanawake huuza miili yao au kusambaza video za ngono ili kupata wateja. Vilevile, kuna usambazaji wa filamu na maudhui mengine yanayopaswa kulipiwa, lakini hupakuliwa bila malipo, jambo linalokiuka haki za wamiliki wa kazi hizo. Aidha, wahalifu hutumia Telegram kusambaza ujumbe na kupanga vitendo vya kihalifu. Kwa ujumla, shughuli nyingi zinazofanyika kupitia jukwaa hili ni kinyume na sheria.
Sababu kubwa ya hali hii ni kwamba Telegram ni jukwaa huria linalotoa kiwango kikubwa cha usiri, hivyo kuficha utambulisho wa watumiaji wake na kufanya iwe vigumu kuwatambua au kuwafuatilia wanaokiuka sheria.
Hata hivyo, pamoja na changamoto hizo, Telegram ni jukwaa zuri la kidijitali lenye manufaa makubwa, hasa katika kulinda faragha ya watumiaji. Ni muhimu kwa jukwaa hili kujiimarisha zaidi kwa kudhibiti vitendo vya kihalifu kwa kuweka mifumo madhubuti ya kutoa taarifa (reporting), ufuatiliaji na udhibiti wa maudhui hatarishi, ili liwe mfano bora wa jukwaa salama katika nyanja ya usalama mtandaoni.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama