Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online-Nkasi
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Dkt. James Kilabuko amezindua nyaraka za usimamizi wa maafa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa huku akisisistiza nyaraka hizo kutekelezwa kwa vitendo.
Dkt. Kilabuko amefanya uzinduzi huo Januari 27, 2026,ambapo amesema hatua hiyo ni mwanzo wa kuanza kazi rasmi endapo kutatokea janga lolote huku akitoa wito kwa idara, vitengo na taasisi ngazi ya Wilaya kuzingatia nyaraka hizo kwa kuhakikisha zinakuwa chachu ya kuongeza ushirikishwaji wa jamii na wadau katika masuala ya menejimenti ya maafa.
Ameongeza kuwa, hatua hiyo itasaidia kujenga uelewa wa jamii kuhusu masuala ya usimamizi wa maafa, kuimarisha mfumo wa utoaji wa tahadhari awali, kujenga uwezo wa kuzuia, kupunguza madhara na kujiandaa na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea.
Amesema nyaraka hizo zimekuja wakati sahihi kwa kuzingatia kuwa Wilaya hiyo imekuwa ikikabiliwa na maafa yanayosababishwa na upepo mkali,magonjwa ya mlipuko kwa binadamu na wanyama, mafuriko pamoja na mgongano wa wanyamapori na binadamu ambayo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara.
“Matokeo ya tathmini ya maafa iliyofanyika katika Halmashauri ya hii Januari, 2026 yalionesha kuwa yapo majanga mengine ambayo yamekuwa yakijitokeza japo hayajaleta athari kubwa ikiwemo wadudu waharibifu wa mazao, ajali za barabarani,majini na moto,tetemeko la ardhi, radi pamoja na maporomoko ya ardhi,”amesema Dkt.Kilabuko na kuongeza:
“Pia natambua kuwa Wilaya hii imekuwa ikikabiliwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu,nitumie fursa hii kuwapongeza kwa jitihada mnazoendelea nazo katika kukabiliana na ugonjwa huo,”.
Vilele alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha kuendelea kuchukua jitihada mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kujikinga na ugonjwa kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu.
Sambamba na hayo, amesema kuwa uandaaji wa nyaraka za usimamizi wa maafa ni hatua nzuri kueleka katika ujenzi wa jamii iliyo stahimilivu dhidi ya majanga katika Wilaya ya Nkasi hivyo ni wajibu wa kila Idara, Vitengo na Taasisi zote zilizopo katika Halmashauri kuzingatia dira hiyo katika kutekeleza vipaumbele vya kisekta.
Dkt. Kilabuko Ameshukuru Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) kwa ufadhili ambao umewezesha kuchangia jitihada za Serikali katika kuandaa mpango wa kujiandaa na kukabiliana na maafa pamoja na mkakati wa kupunguza vihatarishi vya maafa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.
Naye Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu,Brigedia Generali Hosea Ndagala amesema idara hiyo imekuwa ikichukua hatua za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Amesema,serikali kwa kutambua hilo na katika kuhakikisha nchi inakuwa stahimilivu dhidi ya maafa, imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuweka utaratibu mzuri wa kushughulikia masuala ya maafa kwa kutunga Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004, Toleo la Mwaka 2025 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Sura ya 242 ambayo imeweka mfumo mzuri wa usimamizi wa maafa kutoka ngazi ya Taifa hadi Kijiji/Mtaa.
“Ni muhimu kwa Halmashauri kuendelea kutenga fedha katika bajeti juu ya utekelezaji wa mpango huu uliozinduliwa na kuendelea kutoa elimu kuhusu namna bora ya wananchi kuendelea kuchua hatua za awali kwa kuzingatia kuwa maafa ni suala mtambuka na linaanza na mtu mmoja.
“Wananchi waelimishwe kuhusu upandaji wa miti na ujenzi bora unaozingatia viwango ili kuendelea kukabili majanga ikiwemo ya upepo mkali kwa halmashauri,mpango huu uwekwe kwenye utekelezaji na kuwa tayari ili kupunguza madhara, kulinda mali, miundombinu na kuwa na jamii stahimilivu dhidi ya majanga,”amesisitiza Brig Jenerali Ndagala.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijualikali,amesema wilaya hiyo imepata kitu chema kitakachowafaa.
“Nasi tunaahidi kuzitumia kama miongozo sahihi ya kuleta matokeo kwa kuzingatia Serikali imeweka fedha katika kuhakikisha mipango inaleta matokeo yaliyokusudiwa, hivyo tusiwe nyuma, tufanyie kazi kwa tija ya halmashauri nzima,”amesema Lijualikali.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Nkasi Richard Masai,ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhali za awali na kuzingatia taarifa za tahadhali zinazotolewa na wataalamu ili kuendelea kuwa na jamii iliyo salama na yenye kujiletea maendeleo yake.

More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani