Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Dar
Katika kipindi cha siku 100 za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Kata ya Kisukuru iliopo jijini Dar-es-Salaam imekuja na mkakati maalum wa kutokomeza ufaulu wa daraja sifuri (division zero) katika sekta ya elimu ili kuongeza ufaulu katika shule za Serikali.
Diwani wa Kata ya Kisukuru,Lucy Lugome, ameyasema hayo jijini Dar-es -Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari,amesema Kata hiyo ina shule ya msingi moja ambayo ni Magoza na sekondari moja ya Magoza,hivyo mkakati huo umeanza kutekelezwa zaidi katika shule ya sekondari kwa wanafunzi wa kidato cha nne.
Amesema baada ya kupitia matokeo ya miaka mitano iliyopita, ilibainika kuwa ufaulu ulikuwa unapanda na kushuka, hali iliyowasukuma kutumia kipindi cha siku 100 za Rais kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha matokeo, ikiwemo kupunguza division four na kuongeza ufaulu wa jumla katika shule za serikali.
“Utekelezaji wa mkakati huu umeanza kwa kuitisha vikao vya pamoja kati ya walimu na wazazi wa wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne,binafsi nita gharamia mitihani yote itakayofanyika ili kufuatilia maendeleo ya wanafunzi na kuwajengea ari ya kufanya vizuri,”amesema Lugome.
Ameongeza kuwa walimu wameanza kufanya tathmini ya matokeo ya kila mwezi kwa wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne, hatua inayolenga kuwajengea wanafunzi kujiamini na kujiandaa vyema kwa mitihani ya taifa.
Pia amesema wamejipanga kukabiliana na changamoto ya utoro shuleni kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanya doria na kutoa elimu kwa wanafunzi.
Katika sekta ya afya, Lugome amesema wanamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha ujenzi wa hospitali ya ghorofa tatu itakayogharimu shilingi bilioni tano, ambapo taratibu zote za awali tayari zimekamilika.
Amesema ujenzi wa hospitali hiyo unatarajiwa kuanza rasmi katika awamu hii ya uongozi 2025/2030, hatua itakayoboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa Kata ya Kisukuru na maeneo ya jirani.
Pia amesema kata hiyo imefanikiwa kupata jengo halali la serikali kwa ajili ya ofisi za kata, baada ya awali kutumia jengo la kupanga, hali itakayoongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Lugome amesema licha ya changamoto za awali za marejesho tangu mwaka 2017, kwa sasa baraza la kata limeanza kujadili mikakati ya kuhakikisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wananufaika zaidi na mikopo ya asilimia 10.
Ameongeza kuwa tayari baadhi ya vikundi vya vijana wa bodaboda vimepata mikopo ndani ya siku 100 za Rais Samia, huku akisisitiza kuwa juhudi zinaendelea kuhakikisha mikopo hiyo inawafikia zaidi wajasiriamali wadogo wakiwemo akinamama na vijana ili kuleta tija kwa wananchi wa Kata ya Kisukuru.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi