September 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polepole achambua hoja tano zinazopotoshwa na wapinzani

Na Penina Malundo, TimesMajira Online, Dodoma

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi CCM,Humphrey Polepole ametoa msimamo wa Chama chao na kufafanua baadhi ya hoja ambazo zimekuwa zikipotoshwa na baadhi ya vyama upinzani hususani kwa usafiri.

Hoja hizo zimekuwa zikipotoshwa na vyama pinzani katika kampeni wanazozifanya kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia
kufanyika Oktoba 28, 2020.

Akizungumza leo Mkoani Dodoma, Polepole amesema baadhi ya vyama vya siasa vimetumia kampeni kama wigo wa kusema
uongo katika kufanya upotoshaji kwa wananchi.

Amesema, yapo mambo ambayo vyama hivyo pinzani vimekuwa vikipotosha umma hivyo anatoa chama hicho kinatoa elimu juu ya kazi zilizofanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.

Hoja ya Ndege
Polepole amesema kwa Shirika la Ndege (ATCL) kuwa hadi mwaka 2015/16 shirika hilo lilikuwa hoi kifedha na lilikuwa
likijiendesha kwa hasara.

Pia amesema Shirika hilo lilikuwa na ndege moja ambayo ni mbovu,ndani ya miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano zilinunuliwa ndege 11 ambapo hadi sasa nane zimeshawasili nchini.

“Chama cha Lissu kinasema ATCL haikuwahi kukaguliwa naomba tunapozungumza vitu tuwe na uhakika kwa kuwa kila kitu kipo kwenye maandishi na kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) aliyepita lilipata hati safi,”amesema na kuongeza

“Kuhusu hoja ya kuwa ndege zilinunuliwa bila kuidhinishwa katika bajeti ya taifa alimkumbusha katika mazungumzo ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania taarifa muhimu za bunge ’hansard’ zinaonyesha kati ya Juni 2016 hadi Juni 2018 namna wabunge walivyokuwa wakijadiliana juu ya kununuliwa ndege na fedha zikatengwa,”amesema

Amesema, anashangazwa na viongozi wa chama chake wanamuacha vipi mgombea wao anazungumza vitu vya uongo hata kama alikuwa anaumwa maana takwimu zipo na nyaraka zipo kama akitaka atuulize tumueleze lakini si kupita na kusema uongo.

Akitolea mfano wa umuhimu wa kuanzisha mashirika ya ndege na uamuzi mgumu, Polepole alimtaja mtawala wa Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Mfalme Mohamed bin Rashid Al Mktoum ambapo mwaka 2001 alifanya uamuzi wa kununua ndege 56 kwa wakati mmoja.

“Al Maktoum alipata kusema hakuwahi kufanya uamuzi mgumu katika maisha yake kama huo, lakini leo tunaona duniani shirika la ndege linaloongoza kwa ukubwa duniani ni
Emirates, hivyo, hata Rais Magufuli kwa uamuzi wa kununua ndege wapo wanaombeza lakini watakuja kumkumbuka
baadae,” amesema

Wajasiriamali wadogo
Polepole amesema wapo wanaotaka kuwagombanisha wafanyabiashara hao na serikali lakini watambue wafanyabiashara hao walitoka nao mbali.

“Dkt. Magufuli ndiye aliyewaondolea unyonge kinamama waliokuwa wanabeba ndizi kichwani, vijana wanaouza madafu barabarani na mama lishe wanaouza chakula sokoni, walikuwa wakitozwa zaidi ya Sh 180,000 kwa mwaka lakini kwa sasa wametakiwa kulipia Sh 20,000 kwa mwaka ili kuondokana na changamito hiyo,”amesema

Barabara
Polepole amesema wametengeneza barabara kwa kiwango kikubwa,na zipo barabara ambazo zipo katika ilani ya mwaka 2020 -2025 na tayari zimeshaanza kufanyiwa maboresho ikiwemo Barabara ya Mbeya hadi Itigi zaidi ya kilometa 300 ambapo itatengenezwa kwa lami naitakuwa imefunguliwa Mkoa wa Singida na Mbeya na kuachilia fursa nyingi za kiuchumi.

Pia amesema ipo barabara ya kutoka Tabora hadi Mpanda kilometa zaidi ya 300 itafunguliwa ili wananchi wanaoishi kando kando iwe rahisi ya wao kupata fursa ya kufika maeneo mengine kupeleka bidhaa biashara kuachilia fursa za kiuchumi katika maeneo hayo.

“Barabara ya kutoka kigoma Uvinza hadi Mpanda hiyo nayo mkandarasi wapo njiani kuendelea na utengenezaji pia ipo barabara ya kutoka Nyakanazi hadi Manyovu,” amesema.

Reli
Polepole amefafanua kuwa imefanyiwa kazi kubwa ikiwemo reli ya kati ambayo imekuwa kongwe chini ya awamu ya tano reli hiyo ilifanyiwamaboresho kwa kuongezwa uzito wa reli kutoka uzito 50 hadi kufikia 80 na kuwezesha gari moshi kukimbia kwa
wastani kilometa 70/80 kwa saa.

Amesema hiyo itasaidia watu wanaosafiri kutoka maeneo tofautitofauti kufika kwa haraka ambapo mwaka 2014/15 gari moshi ya reli hiyo ilikuwa inakimbia kwa kilometa
15 kwa saa.

“Uboreshaji huu umefanyika kutoka Dar es Salaam ,Isaka ,Kigoma ,kaliua hadi Mpanda ambapo reli imepandishwa kwa uzito 60 kwa Mkoa wa katavi eneo la Mpanda,”amesema

Polepole amesema pia wamefungua reli ambazo hazikuwepo kabisa kati ya miaka 20 iliyopita ikiwemo Tawi la kaskazini kutoka ruvu hadi Moshi ambpo ipo treni ya abiria na ya mizigo.

Amesema wamesogeza sekta wezeshi katika ukuaji wa uchumi mkubwa kwa kusafirisha abiria na mizigo yao hii inachachusha ukuaji wa uchumi katika nchi.

Aidha amesema pia upo mradi wa reli ya umeme ambapo imetoka Dar es Salaam hadi Mkutupola kwa awamu ya kwanza na ya pili ni kutoka Mwanza hadi Mkutupola tayari
fedha imetengwa na kazi inaendelea ya kutengeneza reli hiyo.

Meli
Polepole amesema wameweka Meli katika ziwa Nyasa, Tanganyika na Victoria katika kuwarahisishia wananchi usafiri vizuri na mizigo kusafirishwa kwa bei nafuu.

Amesema usafiri huo umeweza kusaidia kuokoa fedha za wafanyabiashara ambazo walikuwa wanalipa kiasi kikubwa cha fedha katika kusafirisha mizigo yao.

“Tumekarabati meli za abiria na mizigo ili kusaidia watu kuwarahisishia usafiri katika kufanya shughuli zao,”amesema