October 1, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa: Chagueni viongozi watakaowaletea maendeleo

Daud Magesa na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Kwimba

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewakata wananchi wa Jimbo la Kwimba kuchagua viongozi watakaoyaendeleza mambo mbalimbali ya maendeleo yaliyofanyika na kuyaendeleza kwenye maeneo ambayo maendeleo hajafika ili wanufaike zaidi.

Kiongozi huyo ametoa kauli hiyo katika mkutano wa kampeni wa kumuombea kura mgombea Urais wa CCM, Dk. John Magufuli uliofanyika kwenye Kijiji cha Hungumalwa Wilayani Kwimba.

Akiomba kura za Rais Magufuli, Majaliwa amesema, amekuja na mzigo mzito wa kuwaambia wananchi wa Kwimba kupiga kura ili kuchagua kiongozi mwenye uwezo wa kuleta maendeleo kwa Watanzania wenye dini na makabila yote bila kujali itikadi za vyama vyao.

Amesema, wanachotakiwa ni kumchagua Dkt. Magufuli kutokana na sifa za uchapakazi, uadilifu, ushupavu, ujasiri na mwenye upendo wa kuwatumikia wanyonge kwa haki bila ubaguzi wala upendeleo.

“Serikali imefanya mengi ya maendeleo hapa Kwimba, kilichobaki ni kuchagua viongozi wa kuleta maendeleo kule kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa ili wananchi wanufaike,” amesema Majaliwa na kuongeza.

“Urais si kazi ya majaribio,tunatafuta kiongozi wa kuleta maendeleo,maendeleo tunayoyaona yote hayo yameletwa na Dkt. John Magufuli hivyo tukifika hatua hiyo wananchi wa Kwimba, siku ya kupiga kura msimamo wetu ubaki kwa Rais Dk.Magufuli mpeni mitano mingine maana utakuwa peke yako chumbani,”.

Amesema, wananchi wana kila sababu ya kumchagua tena mgombea Urais huyo wa Chama tawala ili aendelee kuleta maendeleo na kuyakamilisha kwenye maeneo mengine ambayo hayajafikiwa.

Alifafanua kuwa hospitali ya zamani ya Wilaya ya Kwimba imeboreshwa na inajengwa nyingine mpya kuhakikisha afya za wananchi zinaimarika ili wafanye shughuli za uzalishaji, kiuchumi na maendeleo.

Mbali na kumwombea kura mgombea urais aliwaombea pi wagombea ubunge na udiwani akisema utatu huo ni betri tatu kwenye kurunzi ya CCM utakaoiwezesha kuwaka, wakikosea na kuchanganya betri haitawaka na hivyo wasifanye makosa Oktoba 28, mwaka huu.

Kwa upande wake Shanif Mansoor, mgombea ubunge wa Kwimba, amesema, Serikali ilileta fedha nyingi za miradi ya jamii miaka mitano iliyopita na ilitekeleza kwa ufanisi ilani ya uchaguzi kwa kujenga nyumba za walimu, barabara, vituo vya afya, hospitali ya wilaya, miradi saba ya maji na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) ili kuzalisha mafundi wa fani mbalimbali.

Miradi hiyo ya maji ni Jojilo, Shinembo, ujenzi wa matenki ya maji Mahiga na Mwang’alanga, ulazaji wa mabomba ya maji Bupandwa na Dodoma pamoja na ujenzi wa tenki la kuhifahi maji lita milioni 2 mjini Ngudu na kuahidi maeneo ya vijijini ambayo hayakupata nishati hiyo watapatiwa ili umeme Kwimba ibaki kuwa historia.

“Serikali ya Rais John Magufuli imekuwa ya historia, imeboresha majengo 12 ya shule Mwamashimba, gari jipya la wagonjwa, mashine ya kufua nguo za wagonjwa na X-ray mpya,jingo la mama na motto, huduma ya macho imejenga hospitali mpya ya wilayana imetoa ten ash. milioni 900,” amesema Mansoor.

Amesema kuwa, wananchi wa Kwimba wanahitaji nafuu ya usafiri hivyo barabara ya Hungumalwa-Nyamilama-Magu itajengwa kwa kiwango cha lami,km 1.2 mjini Ngudu zimejengwa kwa lami bado ahadi ya km 5 ambapo serikali imeboresha barabara kuu ya Mwabuki-Nyamilama-Mwankulwe .

Pia ameomba serikali kujenga soko la kisasa Hungumalwa liwasidie wakulima kupata soko la mazao yao yakiwemo ya mboga mboga na matunda, changamoto ya vituo vya afya kwa wananchi Hungumalwa na Mwakilyambiti ili kuwasogezea karibu huduma za matibabu.