Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online-Nkasi
Umoja wa watu waliosoma katika shule ya msingi Mtenga wajulikanao ” Mtenga we are together”wametoa madawati 20 yenye thamani ya zaidi ya milioni 1.8 na kuyakabidhi shuleni hapo kama sehemu ya kupunguza tatizo la uhaba wa madawati katika shule hiyo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo Januari 20,2026 mwakilishi wa umoja huo Alexander Kapele,amesema kuwa wao kama watu waliowai kusoma katika shule hiyo wametengeneza umoja wa kusaidiana katika shida na raha na wakaona ipo haja kwao kusaidia shule hiyo walau kwa madawati hayo.

Amesema kuwa umoja huo wenye wanachama 40 waishio katika mikoa mbalimbali hapa nchini walihafiki wazo hilo na kuamua kutengeneza madawati hayo ili kuweza kupunguza tatizo la uhaba wa madawati katika shule hiyo na watoto waweze kusoma katika mazingira mazuri na salama.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo,Osiana Mgala, ameushukuru umoja huo kwa kuikumbuka shule hiyo na kuweza kutoa msaada huo ambao anaamini utawasaidia watoto waliokuwa wakikaa chini .
Amesema shule hiyo ina wanafunzi 1,327 huku ikiwa na uhaba wa madawati 251 ambapo mahitaji ni 456 na yaliyopo ni 205,hivyo amewaomba wadau wengine kusaidia shule hiyo.
Mwenyekiti wa kamati wa shule hiyo Patrick Dominico, amewaomba wadau hao wasichoke kusaidia kama hivyo pale watakapokuwa wanapata uwezo kwani shule hiyo bado ina changamoto ya madawati na uchakavu wa baadhi ya majengo na kuwa inahitajika nguvu kubwa katika kurekebisha miundombinu hiyo.
Ofisa Elimu wa Kata ya Mtenga,Benedicto Msesa,amedai kuwa jambo hilo lililofanywa na Mtenga we are together ni la kuigwa kwa Watu wote na kama mawazo hayo yataambukizwa kwa makundi mengine ya kijamii italeta faraja kubwa kwa jamii nzima ya kata ya Mtenga.



More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina