Na Joyce Kasiki
TANZANIA imeendelea kung’ara katika ramani ya dunia ya teknolojia baada ya Benki ya Dunia (World Bank – WB) kuitaja kuwa miongoni mwa nchi zilizo na ukomavu wa juu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika sekta ya umma.
Hatua hiyo inathibitisha mafanikio ya mageuzi ya kidijitali yanayoendelea kutekelezwa na Serikali.
Kwa mujibu wa Ripoti ya GovTech Maturity Index (GTMI) ya mwaka 2025, Tanzania imeorodheshwa katika Kundi A – Ukomavu wa Juu wa Matumizi ya TEHAMA (Extensive GovTech Maturity), kundi linalojumuisha nchi zinazoongoza duniani katika matumizi ya teknolojia kuboresha utoaji wa huduma za serikali na ushirikishwaji wa wananchi.
Ripoti hiyo ya Benki ya Dunia hutathmini kiwango cha ukomavu wa matumizi ya TEHAMA serikalini katika takribani nchi zote duniani, kwa kuzingatia maeneo mbalimbali yakiwemo sera, sheria, miongozo, mifumo ya TEHAMA na utekelezaji wake.
Ripoti ya mwaka 2025 ilitolewa rasmi mwezi Desemba ambapo Tanzania imejirudia katika mafanikio ya Kidunia ambapo hii ni mara ya pili kwa Tanzania kutambuliwa na Benki ya Dunia kwa kupiga hatua kubwa katika ukomavu wa TEHAMA.
Mwaka 2022, Tanzania ilitajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri zaidi duniani katika GovTech Maturity Index, ambapo kati ya nchi 198 zilizoshiriki, ilipanda kutoka nafasi ya 90 mwaka 2021 hadi nafasi ya 26 mwaka 2022, na kutoka Kundi B hadi Kundi A.
Barani Afrika, Tanzania ilishika nafasi ya pili baada ya Mauritius, huku ikiongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki, jambo lililoipa heshima kubwa katika utekelezaji wa mageuzi ya kidijitali serikalini.
Kuimarika kwa nafasi ya Tanzania Kimataifa
Mafanikio haya ni mwendelezo wa safari ya Tanzania ya kupanda ngazi katika matumizi ya TEHAMA serikalini, na yamechangia kuijengea nchi taswira chanya kimataifa na kikanda.
Kupitia matumizi ya teknolojia, Tanzania imeongeza ufanisi wa taasisi za umma, kuimarisha uwazi, na kukuza uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa mujibu wa ripoti ya GTMI 2025, Tanzania ni miongoni mwa nchi tano pekee barani Afrika zilizofanikiwa kuingia katika Kundi la Juu la Ukomavu wa TEHAMA Serikalini.
Nchi nyingine ni Kenya, Misri, Uganda na Rwanda
Maeneo Makuu ya Tathmini ya GTMI
Ripoti ya GovTech Maturity Index 2025 imejikita katika tathmini ya maeneo makuu manne ambayo ni Mifumo ya Mikuu ya Serikali (Core Government Systems),Utoaji wa Huduma za Umma Mtandaoni (Online Public Service Delivery),Ushirikishwaji wa Wananchi Kidijitali (Digital Citizen Engagement),mazingira Wezeshi ya GovTech (GovTech Enablers)
Mifumo Mikuu ya Serikali yachochea Mafanikio
Benki ya Dunia imeeleza kuwa mafanikio ya Tanzania yametokana kwa kiasi kikubwa na uwepo na matumizi madhubuti ya Mifumo ya Mikuu ya Serikali.
Mifumo hiyo ni pamoja na Mfumo wa Taarifa za Watumishi na Mishahara (HCIMS), Ajira Portal, pamoja na mifumo ya kuunganisha na kubadilishana taarifa baina ya taasisi za umma.
Mfumo mkuu wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (GovESB) umetajwa kuwa mhimili muhimu unaowezesha mifumo ya taasisi mbalimbali kusomana na kubadilishana taarifa kwa usalama na ufanisi, hali iliyopunguza urudufu wa taarifa, kuharakisha huduma na kuongeza uwajibikaji.
Ushirikishwaji wa Wananchi Kidijitali
Katika eneo la ushirikishwaji wa wananchi kidijitali, Tanzania imeendelea kuchukua hatua madhubuti kupitia mifumo kama e-Mrejesho, unaowawezesha wananchi kutoa maoni, malalamiko, ushauri na pongezi, pamoja na kupata mrejesho kwa wakat
Mfumo huu umeimarisha uwazi, uwajibikaji na imani ya wananchi kwa Serikali.
Mazingira wezeshi na huduma Mtandaoni
Ripoti imebainisha kuwa uwepo wa sera, sheria, kanuni, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao umeweka mazingira rafiki ya utekelezaji wa miradi ya TEHAMA.
Aidha, utoaji wa huduma mtandaoni kupitia mifumo kama GePG, NeST na TAUSI umeongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwa haraka na kwa gharama nafuu
Mtazamo wa e-GA
Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhandisi Benedict Ndomba, anasema hatua hiyo ni ushahidi wa mwelekeo sahihi wa Taifa katika kujenga Serikali ya kidijitali.
Anasema utafiti wa Benki ya Dunia ulifanyika kwa takribani mwaka mmoja kwa kukusanya ushahidi wa matumizi ya TEHAMA serikalini, na kusisitiza umuhimu wa taasisi za umma kuzingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao, pamoja na kuunganisha mifumo yao na GovESB.
Amesisitiza kuwa, uwepo wa mifumo mbalimbali ya TEHAMA serikalini unaonesha usimamizi mzuri wa rasilimali za TEHAMA.
Anatumia nafasi hiyo kutoa wito kwa taasisi za umma kuendelea kuzingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika utekelezaji wa miradi ya TEHAMA. Pia amehimiza matumizi ya mifumo ya ushirikishwaji wa wananchi na kuunganisha mifumo ya taasisi na GovESB.
TEHAMA na Changamoto za Matumizi ya Karatasi
Mtaalam wa Mifumo kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Daniel Ngodya, anaeleza faida za mifumo akisema mifumo hii imeleta mabadiliko makubwa katika kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji na kwamba Taasisi zimeweza kuwahudumia wateja kwa haraka na kwa gharama nafuu zaidi ikilinganishwa na mifumo ya zamani ya kutumia makaratasi na huduma za ana kwa ana pekee.
Anasema mfano mzuri wa mafanikio ya mifumo ya kidigitali ni Mfumo wa Malipo ya Serikali (GEPG) unaotumiwa na taasisi nyingi za umma ambapo kupitia mfumo huo, mteja anaweza kufanya malipo wakati wowote na akiwa mahali popote, mradi awe na simu na salio katika akaunti yake ya simu au benki.
”Hali hii ni tofauti kabisa na miaka 25 iliyopita ambapo ilibidi mteja aende benki, apange foleni ndefu, au aende ofisini kulipa pesa taslimu na kusubiri risiti ya karatasi.”anasema Dkt.Ngodya
Anasema Kwa upande wa taasisi, matumizi ya mifumo ya kidigitali yameimarisha ukusanyaji wa mapato na usalama wa fedha. Urahisi wa malipo umeongeza idadi ya wateja wanaolipa kwa wakati, hivyo kuongeza mapato ya taasisi. Aidha, mifumo imepunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya udanganyifu kama vile utoaji wa risiti feki, kwa kuwa miamala yote inarekodiwa moja kwa moja ndani ya mfumo.
Anataja faida nyingine muhimu ni uwezo wa taasisi kupata taarifa za kifedha kwa wakati halisi. Kupitia mifumo ya TEHAMA, taasisi zinaweza kujua kiasi cha mapato kilichokusanywa ndani ya saa moja au siku moja, jambo linalorahisisha upangaji wa bajeti na mipango ya maendeleo.
Vile vile anasema Utunzaji wa kumbukumbu pia umeimarika kwa kiwango kikubwa kupitia matumizi ya mifumo ya kidigitali. Taarifa nyingi sasa zinahifadhiwa kama nakala laini ,hali inayorahisisha uhifadhi wa muda mrefu, upatikanaji wa haraka wa taarifa, na kupunguza gharama za kuhifadhi makaratasi na hivyo kuongeza usahihi wa taarifa na kupunguza makosa yanayotokana na uingizaji wa taarifa kwa mkono.
Kuhusu changamoto za awali kabla ya mifumo anasema, matumizi ya karatasi yana changamoto nyingi ikiwemo athari za kimazingira kutokana na ukataji miti, ukosefu wa ufanisi katika uchakataji wa taarifa, changamoto za usalama wa taarifa, pamoja na ugumu wa uhifadhi na upatikanaji wa taarifa kwa wakati.
Wananchi Wapongeza Mageuzi ya Kidijitali
Baadhi ya wananchi wamepongeza hatua ya Serikali kutumia mifumo ya TEHAMA wakisema imeleta urahisi mkubwa katika maisha yao ya kila siku.
Athonia Alphonce, mkazi wa Mailimbili jijini Dodoma, amesema matumizi ya mifumo yamesaidia pia utunza mazingira kwa kupunguza matumizi ya karatasi.
Kwa upande wake, John Raphael mkazi wa Uhindini jijini Dodoma, anasema mifumo ya kidijitali imeokoa muda na gharama kwa wananchi kwani huduma nyingi sasa zinapatikana moja kwa moja kupitia simu za mkononi bila kwenda ofisini, ikiwemo malipo ya umeme na maji.
Mafanikio haya kwa ujumla ,yanaifanya Tanzania kuwa kielelezo cha mageuzi ya kidijitali barani Afrika, na kuweka msingi imara wa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za umma, kukuza uwazi, kulinda mazingira na kuimarisha uchumi wa kidijitali kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina