Na Esther Macha, TimesmajiraOnline,Mbeya
KATIKA tukio lililoibua shangwe na hisia miongoni mwa wazazi na wanafunzi, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) kupitia Mkoa wa Mbeya,Ndele Mwaselela amejitolea kuwalipia walimu wa masomo ya ziada katika Shule ya Sekondari Malama, hivyo kuondoa kabisa michango iliyokuwa ikitolewa na wazazi.
Hatua hiyo imewanufaisha wanafunzi wa madarasa ya mitihani ya Kidato cha Pili na Kidato cha Nne katika shule hiyo iliyopo Mji mdogo wa Mbalizi, Kata ya Nsalala, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.
Akizungumza Januari 16, 2026 shuleni hapo wakati wa hafla ya kukabidhi meza 200 na viti 200 Mwaselela amesema kuanzia sasa gharama zote za masomo ya ziada zitalipwa na Paradise Mission bila mzazi yeyote kuchangishwa fedha.

“Walimu wa Kidato cha Pili na Nne watalipwa na Paradise Mission kwa ajili ya masomo ya ziada. Mzazi yeyote asichangishwe tena. Najua maisha ya wazazi wengi ni magumu, nami nililelewa na mama muuza mboga, hivyo naelewa changamoto zao,” amesema Mwaselela.
Amesisitiza kuwa kuanzia mwezi Februari, 2026, ni marufuku kwa wazazi kuchangishwa fedha kwa ajili ya masomo ya ziada, akisema hiyo ni sehemu ya maelekezo ya Chama cha Mapinduzi ya kuhakikisha elimu inapatikana bila mzigo kwa wananchi.
Mwanafunzi wa shule hiyo,Bakari Yusuph, ameseema uamuzi huo umepunguza kwa kiasi kikubwa mzigo kwa wazazi na kuwapa wanafunzi fursa ya kusoma kwa utulivu.
“Wazazi wengi hawakuwa na uwezo wa kulipa fedha hizo. Tunamshukuru MNEC Mwaselela na tunaahidi kusoma kwa bidii ili kumlipa kwa matokeo mazuri,” amesema Bakari.
Kwa upande wake, Sabina Salanda mkazi wa Kitongoji cha Mapinduzi, amesema msaada huo umeleta faraja kubwa kwa wazazi wengi.
“Hatujui cha kumlipa. Maisha ni magumu, lakini alichokifanya ni kikubwa sana kwetu. Ametugusa hadi machozi,” amesema mzazi huyo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Njile Dinday, amempongeza Mwaselela kwa kuendelea kuunga mkono sekta ya elimu wilayani humo, akisema mchango wake umekuwa na manufaa makubwa kwa shule mbalimbali.
Ameahidi kuwa halmashauri itaendelea kushirikiana na wadau wote wa maendeleo kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, huku akimuomba Mwaselela kuendeleza moyo huo wa kusaidia elimu.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi