March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Namna mwanamke atajiepusha na saratani ya mlango wa kizazi

*Wanawake wanaojamiiana wako hatarini

Na Mwandishi Wetu

Januari kila mwaka ni kipindi ambacho wanawake kote duniani huutumia kwa ajili ya kupata elimu juu ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi, ambayo ndiyo inayoongoza kwa vifo vingi hapa nchini.


Asasi ya Shujaa Cancer Foundation (SCF) kwa kushirikiana na redio ya Wanawake ya Malikia Choice FM inatekeleza maadhimisho hayo kwa kutoa fursa ya wanawake kupata uchunguzi wa saratani hiyo bila malipo pamoja na kupata elimu na ushauri.


Mkurugenzi Mtendaji wa SCF, Gloria Kida anasema saratani ya mlango wa kizazi inayoongoza kwa vifo vingi hapa Tanzania, ambapo inakadiriwa kuwa kila mwaka wanawake zaidi ya 10,000 huugua na kati yao 6,000 hufariki dunia.


“Jamii inapaswa kufahamu kuwa saratani ya mlango wa kizazi ni ugonjwa unaoweza kuzuilika na kutibika kirahisi pale inapogundulika katika hatua za awali.Ni bahati mbaya kwamba wanawake wengi wanakuwa na woga wa kuchunguza saratani hii jambo ambalo linawafanya waende kupata huduma hospitalini kwa kuchelewa,”anasema na kuongeza:

“Wengi huenda hospitalini wakiwa tayari na hali mbaya, yaani hatua ya tatu na ya nne. Hali hiyo ndiyo inayosababisha wengi wao kupoteza maisha maana tiba inakuwa ngumu huku gharama ikiwa kubwa.


“Nawashauri wanawake wenzangu kuchunguza saratani hii kila mwaka kama njia muhimu ya kuwaepusha kutumia gharama kubwa za matibabu na hata vifo,” anaonya Kida.


Anasema katika maadhimisho ya mwaka huu, wamekusudia kutekeleza maazimio ya Shirika la Afya Duniani (WHO) la kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 asilimia 90 ya wanawake wamechanjwa kikamilifu chanjo ya HPV watimizapo umri wa kuweza kujamiina wa miaka 15, kuboresha vipimo vya saratani ya mlango wa kizazi na wanaogundulika wanapata matibabu sahihi.


Anasema maambukizi ya virusi vya HPV ndiyo yanayosababisha saratani ya mlango wa kizazi na mwanamke anaweza akaishi na maambukizi kwa miaka 20 bila kuonesha dalili zozote za wazi hadi atakapofanya uchunguzi hospitalini.


“Tunaomba wanawake wote kufanya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi, angalau kila mwaka na wale wenye umri kati ya miaka tisa hadi 14 wapate chanjo ya HPV inayotolewa bure katika vituo mbalimbali vya afya nchini,”ameshauri Kida.


Katika maadhimisho ya mwaka huu anasema wanashirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) katika kutoa uchunguzi wa saratani hiyo bure kwa wanawake jijini Dar-es- Salaam na kuwapa elimu ya ufahamu wa ugonjwa huo pamoja na namna ya kuuepuka.

Dkt. Handali Samweli kutoka Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani ORCI anasema kuwa tafiti mbalimbali za taasisi hiyo zinaonesha kuwa saratani ya mlango wa kizazi huwaathiri wanawake kati ya umri wa miaka 25 hadi 50 na inachangia asilimia 60 za wagonjwa wanaotibiwa kwenye taasisi hiyo.


“ORCI hupokea wagonjwa kati ya 25 hadi 30 kwa wiki wenye saratani ya mlango wa kizazi. Asilimia 80 hufika hospitalini wakiwa katika hali mbaya inayotoa ugumu wa tiba, hivyo mgonjwa hupewa matibabu ya kupunguza makali. Ni vyema wanawake kuchunguza mara kwa mara kwa sababu ugonjwa huu hutibika kirahisi unapokuwa katika hatua za awali,” anasema Dkt. Handali.

SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI NI NINI?


Dkt.Handali anasema saratani ya mlango wa kizazi ni mabadiliko ya chembechembe (seli) hai zilizo juu au zinazofunika mlango wa kizazi.

Saratani hii huchukua miaka mingi kujitokeza kati ya miaka 15 hadi 20,lakini kabla ya kujitokeza kunakuwa na mabadiliko yanayojitokea ambayo yanaweza kugundulika mapema na kuzuilika katika hatua hiyo.


Anasema ugonjwa hujitokeza zaidi katika umri kati ya miaka 25 hadi 50 ambapo hii inaweza kuchukuliwa kuwa ni wastani wa miaka 45.


Anataja mambo yanayosababisha ugonjwa wa saratani ni binti kuanza kujiiana mapema chini ya umri wa miaka 18, mwanamke au mwanaume kuwa na mpenzi zaidi ya mmoja, uvutaji wa sigara, historia ya kubeba mimba nyingi na mimba za utotoni chini ya miaka 18.

Mambo mengine anayataja kuwa matumizi ya pombe kwa wingi, virusi vinavyopatikana kwa njia ya kujamiina vinavyojulikana kwa lugha ya kitaalamu kama Human Papiloma Virus (HPV) na walioambukizwa virusi vya Ukimwi wapo hatarini zaidi.

Dkt. Handali anasema dalili za saratani ya mlango wa kizazi huanza kuonekana wakati ugonjwa unapokomaa. Dalili hizo ni kama kutokwa na damu ukeni ambayo si ya hedhi, kutokwa na uchafu, majimaji au usaha na maumivu wakati wa kujamiiana na wakati mwingine huweza kuandamana na utokaji wa damu.

Pia huandamana na maumivu ya tumbo chini ya kitovu au maumivu ya kiuno.
Iwapo saratani itakuwa imefika hatua kubwa husababisha athari kwenye njia ya mkojo na haja kubwa na pia ugonjwa unaweza kwenda kwenye mifupa na kusababisha maumivu sehemu husika.

Ili kuepuka ugonjwa huo, Dkt. Handali anasema wanawake ambao wameshakuwa na mahusiano ya kimapenzi wanapaswa wanapaswa kupima mara kwa mara hadi wanapofika umri wa miaka 69.

Anasema ili mwanamke kuepuka ugonjwa huu inambidi afanye uchunguzi wa mara kwa mara, mke au mume kutokuwa na wapenzi wengi, kutoanza kujamiiana kwenye umri mdogo, kutozaa sana na kutovuta sigara.

Mmoja wa wanawake waliofika kuchunguza saratani ya mlango wa kizazi, Maya Adamu anasema awali alikuwa anasikia uchunguzi hufanyika kwa kunyofoa kinyama kwenye sehemu za siri lakini amebaini hizo ni habari potofu na kwamba hakuna maumivu.

“Tumepewa huduma nzuri. Hakuna maumivu. Unajua huko mitaani tumekuwa na mawazo kwamba unapopimwa saratani ya mlango wa kizazi unanyofolewa nyama sehemu za siri. Lakini sivyo. Wala husikii maumivu. Huduma ni nzuri sana na nawashauri wanawake wenzangu wasihofie kupima.”


Mkurugenzi wa Choice FM, Juhayna Ajmi aliwataka Watanzania kuachana na tabia ya woga wa kuchunguza afya ya uzazi kwa maelezo kwamba “Kuogopa hakusaidii kitu zaidi kuongeza madhara na hata kusababisha kifo wanapochelewa tiba,”.